Uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka – DAWASA

0

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imesema, uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita Milioni 520 kwa siku mpaka lita Milioni 534.6 kwa siku.

Uzalishaji huo, ni sawa na ongezeko la lita Milioni 14.6 kwa siku, ambapo ni pamoja na ongezeko la uwezo wa DAWASA katika kuhifadhi maji, kutoka lita Milioni 153.64 hadi lita Milioni 183.64 sawa na ongezeko la lita Milioni 30.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, alisema hayo wakati akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuelezea mafanikio ya taasisi za Serikali.

Bwire alisema, mbali na ongezeko la uzalishaji maji na uhifadhi, mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji umeongezeka kutoka Kilomita 4,690.7 hadi Kilomita 7,087.

“Mtandao wa majitaka nao umeongezeka kutoka Kilomita 450 hadi Kilomita 517.12, ambalo ni sawa na ongezeko la Kilomita 67.12, huku idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi ikiongezeka kutoka 343,019 hadi 438,177,” alisema Bwire wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Bwire alitumia mkutano huo kuelezea Mradi wa Maji Dar es Salaam ya Kusini, ambao mkataba wake ulisainiwa Oktoba 31, 2023, ambao utakuwa ujenzi wa tenki la ujazo lita Milioni 9, mradi ambao una thamani ya Shilingi Bilioni 34.5.

Wakati huo huo, Mhandisi Mkama Bwire alisema, Mto Ruvu umeendelea kuwa chanzo kikuu cha maji kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambapo wanapata asilimia 87 ya maji wanayozalisha.

Vyanzo vingine ni visima asilimia saba; Mto Kizinga asilimia mbili na Mto Wami asilimia nne, huku kukiwa na jitihada za kuhakikisha mtandao wa Kilomita 7,087 wanaohudumia unakuwa na ufanisi mkubwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi na mamlaka kwa ujumla.

Mhandisi Bwire alisema, DAWASA inatekeleza majukumu makuu mawili ikiwemo kutoa huduma ya maji safi na salama katika maeneo wanayohudumia na kusimamia usafi wa mazingira, “licha ya kutoa huduma mkoani Dar es Salaam, pia tunatoa huduma baadhi ya maeneo Mkoa wa Tanga, Morogoro na Pwani.”

“Katika kuboresha maeneo yetu ya huduma tumegawa mikoa ya kihuduma ya DAWASA takribani 23. Ilani inatutaka ifikapo 2025 tuwe tumefikia asilimia 95 ya huduma ya maji, lakini kwa sasa kwa mwelekeo wamefikia asilimia 93 kutokana na mtandao wa usambazaji maji.

“Kazi kubwa tiliyo nayo ni kuangalia ni kwa namna gani haya maji yanawafikia wananchi,” alisema.

Aliendelea kusema, kuna maeneo ambayo yanapata maji muda wote, mengine kwa kiwango, lakini mengine wapo katika hatua ya kufikisha huduma ya maji ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma ya maji safi na salama.

“Ukienda maeneo ya Kigamboni kuna maji ya kutosha, kinachotakiwa ni kuongeza mtandao wa usambazaji vivyo hivyo kule Mkuranga na kwingineko,” alisema.

Pia, alisema kutokana na vyanzo vya maji walivyo navyo kuonekana kuelemewa wapo mbioni kupata vyanzo vingine vya maji ikiwemo kutoka Mto Rufiji na Bwawa la Kidunda.

Mhandisi Bwire akizungumzia kuhusu Bwawa la Kidunda alisema, lengo la ujenzi wa bwawa hilo ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi kwa kuhakikisha maji katika Mto Ruvu yanapatikana kwa kipindi chote cha mwaka ili kutoa huduma ya majisafi kwa Mikoa ya Dar es Salaam, Kibaha na mji wa Bagamoyo.

“Vile vile kuwezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa matumizi ya majumbani na viwandani, nishati ya umeme na baadaye wanaweza kuangalia namna ambavyo litasaidia katika kilimo cha umwagiliaji,” alisema.

Ujenzi wa bwawa hilo ambao unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita unatarajia kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 300 na Mkandarasi ni Sino Hydro Corporation kutoka China ambaye tayari ameanza utekelezaji wake

Aidha, kukamilika Mradi wa Kidunda utawezesha mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini yenye kuzalisha jumla ya lita Milioni 466 kwa siku, kuwa na uwezo wa kuzalisha maji katika majira yote ya mwaka na hivyo kuepusha upungufu wa maji katika majira ya kiangazi nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here