‘Uuzaji holela sumu za panya ni kosa kisheria’

0

MAMLAKA ya Afya ya mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imeweka wazi kwamba, uuzaji holela wa sumu za kuua wadudu wakiwemo panya na mende ni kosa kisheria.

Akizungumza kwenye Mkutano na Wahariri na Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili Hazina, Kaimu Meneja Kanda ya Mashariki TPHPA Mahamudu Sasamalo alisema wafanyabiashara wa sumu hizo wanapaswa kufuata utaratibu na kupewa vibali vya kufanya biashara hiyo.

Alisema, wameanza kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ili wabadili mfumo wa uuzaji wa sumu hizo za kuulia wadudu mitaani, na baadae wataanza kuchukua hatua ili kudhibiti uuzaji holela.

“Hatuwazuii kuuza, ila wauze kwenye sehemu husika, tumeshaanza kutoa elimu na baadae tutachukua hatua. Tunawaomba wananchi wasinunue sumu hizo kwenye maeneo yasiyohusika,” alisema Sasamalo.

Wananchi mbalimbali waliozungumza na Afrika Leo kwa nyakati tofauti, wamepongeza hatua hiyo ya TPHPA kuzuia uuzaji holela wa dawa za kuulia wadudu mitaani, kwani zinasababisha madhara makubwa ikiwemo watu kuzitumia katika matumizi yasiyo sahihi ikiwemo kujiua au kuwadhuru wengine.

“Naona ni hatua nzuri, kuna haja ya kudhibiti zaidi ununuzi holela wa sumu hizi maana siku hizi taarifa za watu kujiua zinaongezeka na wengi utasikia ni kwa kutumia sumu za panya, hii ni kwasababu zinapatikana kwa urahisi mitaani,” alisema Juma Shamte, mkazi wa Mbagala Zakhiem.

Alisema, mbali na udhibiti huo wazazi na walezi majumbani wanapaswa kuwa makini wanaponunua na kutega sumu hizo, kwani nyingine zinafanana na pipi, hivyo zinaweza kuliwa na watoto na wakapoteza maisha.

“Nawasihi wazazi wenzangu wawe makini sana na hizi sumu wanazonunua, ni lazima wafuate matumizi sahihi na wawe makini wanapozitega au kuzihifadhi, vinginevyo tunaweza kupoteza maisha ya watoto wetu au zinaweza kutumiwa vibaya na watu wenye nia ovu kudhuru familia zetu,” alisema.

Aidha, zipo taarifa nyingine ambazo zimewahi kuripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini zikidai kwamba, wapo vijana mitaani ambao wanatumia baadhi ya sumu za panya kama kilevi.

Inadaiwa, vijana hao wamekuwa wakinunua sumu hizo na kuchanganya na bangi na kuvuta, jambo ambalo ni hatari kwa afya zao, na hivyo Serikali imeshauriwa kuweka nguvu kubwa zaidi kutoa elimu na kudhibiti sumu hizo ili vijana wengi wasiingie kwenye ulevi huo hatari.

Hata hivyo, Tanzania sio nchi ya kwanza kuzuia uuzaji holela wa sumu hizo, nchini Kenya Bodi ya Kudhibiti Kemikali (PCPB), hivi karibuni imepiga marufuku biashara za wachuuzi wa dawa za mende na panya mitaani.

Akinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo, Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi hiyo, Fredrick Muchiri, alisema hatua hiyo inatokana na kukithiri kwa matukio yanayosababishwa na uuzaji holela wa sumu hizo.

“Kwa sasa, tunashughulikia mikakati ya kukomesha uuzaji na uchuuzaji wa dawa za mende na panya mitaani,” alisema na kusititiza kuwa, pamoja na kushughulika na uuzaji huo mitaani, pia wanafanya jitihada za kukomesha chanzo cha uingiaji wa sumu hizo.

“Tunalenga chanzo chake, dawa zinakotoka. Tukiangazia hilo, dawa hizo hazitawahi kuonekana mitaani tena, mchuuzi anaweza akakuuzia chochote, ila sasa umewadia wakati kukomesha uuzaji wa kemikali kiholela. Lazima kuwe na mpangilio,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo la nchini Kenya, hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Shirika moja lisilo la Kiserikali nchini humo kufichua kuhusu kuwepo kwa kemikali hatari hasa za kilimo.

Katika kikao cha awali na waandishi wa habari, kilichoandaliwa na kampuni ya aak-Grow ambayo imeshirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta (KNH) kuzindua upya kituo cha kupokea taarifa za watu kunywa sumu au kuathirika, ilibainika kwamba, wakulima wanatumia Kemikali zilizopigwa marufuku kukuza chakula.

Gazeti hilo lilidai kwamba, kwenye mitaa mingi nchini humo, hasa maeneo ya mijini, wachuuzi wa dawa za mende na panya wanaendeleza biashara hiyo bila kudhibitiwa.

Hatua hiyo inaibua hatari kuhusu usalama wa watu kiafya haswa wanaozinunua, nyingine zikitajwa kuwa bandia na hatari zaidi kwa afya za binadamu, ambapo kwa hapa Tanzania, jukumu hilo linafanywa na Mamlaka ya Afya ya mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA).

TPHPA ambayo ilianza kazi rasmi Julai, 2022, ikiundwa kwa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.4 ya mwaka 2020 (Plant Health Act No. 04 of 2020, moja ya majukumu yake ni kudhibiti uagizaji, usafirishaji, utengenezaji, usambazaji, uuzaji, na matumizi ya viuatilifu na vifaa vya unyunyiziaji wa viuatilifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here