Utekaji ulivyogeuka ajira kwa vijana duniani

0

Na Mwandishi Wetu

WATU wengi hawajui kwamba, yapo matukio mengi ya utekaji yametokea kwenye nchi mbalimbali duniani yakiwahusisha wafanyabiashara matajiri, wanamuziki, waigizaji wenyewe au familia zao. Nchini Nigeria inaelezwa, matukio hayo yameonekana kuwa ya kawaida na utekaji unachukuliwa ni sehemu ya ajira kwa vijana wengi nchini humo.

Vijana wanajitosa kwenye utekaji kwa lengo la kujipatia kipato cha haraka, kwani wamekuwa wakiwateka matajiri na watu wenye uhusiano wa karibu na matajiri hao na kudai walipwe kiasi kikubwa cha fedha. Haya ni baadhi ya matukio ya utekaji yaliyowahi kutokea na kuviteka vyombo vya habari duniani:-

Andre Hanekom 

Huyu ni bilionea kutoka Afrika Kusini, lakini biashara zake anafanyia nchini Msumbiji. Tajiri huyu alitekwa Machi, mwaka 2018, alipokuwa nje ya Hoteli ya Amarula, iliyopo kwenye Mji wa Cabo Delgado. Inasemekana tajiri huyu alitekwa na watu watano wasiojulikana.

Liyaqat Ali Parker

Ni bilionea kutoka Afrika Kusini. Yeye alitekwa Julai 9, 2018 akiwa ndani ya jengo la ofisi zake katika mji wa Capetown. Mfanyabiashara huyu alizuiliwa kwa miezi miwili hadi aliporejea nyumbani kwake mnamo Septemba 17, 2018.

Siku aliyotekwa, wanaume watano wasiojulikana wanadaiwa kulifuata gari lake hadi kwenye maegesho ya maeneo zilipo ofisi zake, baadae watu waliokuwa na silaha, walimshambulia mlinzi wake na kumfungia chooni na pia kumpora simu yake na kumteka mfanyabiashara huyo na kumuingiza ndani ya gari lao kisha wakatokomea kusipojulikana.

Chief Michael Obi

Ni bilionea kutoka Nigeria ambaye pia ni baba wa mcheza mpira maarufu Mikel Obi. Bilionea huyu alitekwa kabla ya mechi ya Kombe la dunia baina ya Nigeria na Argentina. Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa tajiri huyu kutekwa, ambapo Agosti, mwaka 2011 alitekwa kwa mara ya kwanza na kuachiwa.

Ivan Kaspersky

Ivan Kaspersky ni mtoto wa Eugene Kaspersky; tajiri mtengenezaji wa programu za kompyuta na programu za kupambana na virusi vya kompyuta (Anti virus) na kupambana pia na wadukuzi. Mwaka 2011, kundi la watekaji nyara lilifanikiwa kumteka Ivan aliyekuwa na umri wa miaka 20 wakati huo. 

Watekaji hao, walimzuia mtoto huyo kwenye mji wa Moscow na kudai walipwe fedha ili wamuachie, lakini watekaji hao hawakufanikiwa kwenye mpango wao, baada ya wapelelezi kujua walikuwa wanamzuilia wapi kwa kufuatulia mawimbi ya moja ya simu waliyotumia kumpigia baba wa mtoto huyo na kumuokoa.

Shiraz Gathoo 

Ni mfanyabiashara maarufu kutoka Afrika Kusini. Gathoo alitekwa Machi 10, mwaka huu. Watekaji walijifanya kuwa ni askari wa usalama barabarani na kuweka kizuizi bandia barabarani na kumteka. Hata hivyo, aliachiwa huru baada ya kukaa mateka kwa miezi sita, ingawa hadi leo haijajulikana aliachiwa kwa makubaliano gani na watekaji hao.

Sikhumbozo Mjwara 

Sikhumbozo ni mfanyabiashara wa madini na mmiliki wa migahawa anayeishi jijini Durban, Afrika Kusini. Naye alitekwa Agosti na mpaka sasa bado hajulikani alipo. Mfanyabiashara huyu alitekwa akiwa nje ya mahakama ya hakimu mjini Verulam baada ya kuhudhuria kikao cha kusikizwa kwa kesi inayohusisha mzozo wa kifedha. 

John Paul Getty III

Tukio hili linakumbukwa na wengi kutokana na kile kinachoelezwa ni matokeo ya mtu kuwa bahili kupita kiasi. Mwaka 1973, wahalifu walimteka mjukuu wa tajiri huyu wa mafuta Jean Paul Getty, ambaye anajulikana kwa jina la John Paul Getty III. Wakati anatekwa, alikuwa na miaka. Mtoto huyu alitekwa akiwa jijini Roma, Italia.

Watekaji walidai walipwe kiasi kikubwa cha fedha ili wamuachie, fedha hizo inasemakana zilikuwa ni ndogo kulinganisha na utajiri wa babu yake, lakini mzee huyo aligoma kulipa na hilo lilichangiwa na tabia ya mjukuu wake kutania watu kwamba, anaweza kujiteka mwenyewe.

Ndio maana babu huyo alipopewa ujumbe wa kudai atoe fedha kumkomboa mjukuu wake, alipuuza. Isitoshe aliamini kama angelipa fedha hizo, basi angewaweka hatarini jamaa zake wengine, kwani watekaji wangewalenga na kudai fedha.

Watekaji nyara walipoona kuna dalili za kukosa fedha, waliamua kumtumia ujumbe kwamba, wamemkata mjukuu huyo sikio na kutuma kipande chake pamoja na fungu la nywele kwenye gazeti, na waliongeza kuwa iwapo asingelipa fedha walizotaka, wangeendelea kumkata vipande mjukuu huyo kila wakati.

Jambo hilo lilimtisha tajiri huyo na kuamua kulipa kiasi cha fedha walizotaka watekaji hao, ingawa inaelezwa waliongeza kiwango ambacho kilizidi kile cha awali na kumfanya tajiri huyo kujutia maamuzi ya kusita kulipa fedha hizo mapema kabla dau halijaongezwa.

Walter Kwok

Mwaka 1990, Walter Kwok na ndugu zake wawili walirithi mali ya kampuni tajiri zaidi katika biashara ya ardhi na nyumba jijini Hong Kong; Sun Hung Kai Properties pamoja na mali ya baba yao Kwok Tak Seng.

Kutokana na utajiri huo, vijana hao wakaingia kwenye orodha ya Forbes ya watu tajiri zaidi duniani, jambo ambalo liliwaweka kwenye hatari ambapo mwaka 1997 Kwok alitekwa na jambazi maarufu Cheung Tze-keung, maarufu zaidi kwa jina ‘Big Spender’.

Mke wake Kwok, Wendy alifanikiwa kushauriana na watekaji na kufanikisha uhuru wake bila kuwashirikisha polisi. Ingawa hakukuwa na taarifa yoyote rasmi kuhusu kiasi kilicholipwa ili kumkomboa tajiri huyo, ingawa inadaiwa Wendy alitoa kiasi kikubwa cha fedha.

Aldo Moro

Huyu alikuwa mwanasiasa maarufu nchini Italia, aliwahi kuwa Waziri Mkuu kati ya 1963-1968. Moro alikuwa ndiye Waziri Mkuu aliyekaa muda mrefu zaidi kwenye nafasi hiyi tangu wakati wa vita vikuu vya dunia. Lakini umaarufu wake na kupendwa kwake na watu pengine ndio vilichangia hadi akatekwa.

Ilikuwa ni Machi 1978, wanachama wa kundi la wanamgambo wa ‘Red Brigades’ waliwaua walinzi wake watano na kumteka kutoka kwenye barabara moja kwenye jiji la Roma.

Watekaji hao walitaka kuachiliwa huru kwa wenzao 16 waliokuwa wanazuiliwa na serikali ndipo waruhusu kumwachilia Moro jambo ambalo Serikali ilikataa, hivyo baada ya kushikiliwa mateka kwa siku 55, alipigwa risasi mara kumi akiwa kwenye gari na mwili wake kutelekezwa.

Charles Lindbergh Jr.

Tukio hili lilitikisa dunia mwaka 1932. Charles Lindbergh Jr alikuwa mtoto wa rubani maarufu wa ndege Charles Lindbergh ambaye alikuwa pia mwandishi maarufu. Charles Lindbergh alikuwa anatazamwa na wengi kama ‘Shujaa wa Marekani’ baada ya kuwa wa kwanza kufanikiwa kuvuka bahari ya Atlantiki akiwa kwenye ndege peke yake.

Mtoto huyo alikuwa na miezi 20 alipotekwa nyumbani kwao New Jersey. Mtekaji aliacha ujumbe uliokuwa na makosa mengi ya kisarufi, akidai alipwe fedha ili amrudishe mtoto huyo huku akitahadharisha familia hiyo isitangaze jambo hilo wala kutoa taarifa polisi. 

Hata hivyo, taarifa zilienea haraka, licha kuhakikishiwa kwamba mtoto wao angekuwa salama baada ya kulipa fedha, mwili wa mtoto huyo ulipatikana vichakani miezi miwili baada ya kutekwa. Polisi walifanikiwa kumtafuta mtekaji huyo kwa kufuata namba za usajili za dola zilizotumiwa kumlipa, Richard Hauptmann alikamatwa na kupatikana na hatia ya utekaji nyara na mauaji, naye aliuawa kwa umeme mwaka 1936.

George Clooney

Mwigizaji George Clooney alikuwa Darfur, Sudan akiwa na baba yake akiigiza filamu ya ‘A Journey to Darfur’ (Safari ya Darfur), ndipo kundi la watoto waliokuwa na bunduki aina ya AK47 walipowashambulia. Walishambuliwa wakivuka kwenye kizuizi cha barabarani na kuporwa kila kitu kwenye gari lao.

Familia ya Jennifer Hudson

Jennifer Hudson alipata umaarufu aliposhiriki katika kipindi cha American Idol mwaka 2004. Ingawa alimaliza akiwa was aba, nyota huyo alipata umaarufu kutokana na kipaji chake.

Mwaka 2008, alipata pigo kubwa pale mama yake mwenye umri wa miaka 57 Darnell, ndugu yake Jason, 29, na binamu yake Julian, 7, walipozuiliwa mateka na kisha kuuawa kwa kupigwa risasi na mtu anayejulikana kama William Belfour.

Belfour alikuwa mume wa zamani wa dada yake Jennifer Hudson, alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji na uvamizi, akahukumiwa vifungo vitatu vya maisha na miaka mingine 120. Jennifer Hudson na jamaa zake ili kutafuta kitu cha kuwapa matumaini baada ya kisa hicho, walianzisha umoja wa Hudson-King wa familia za watu waliouawa kwenye matukio ya utekaji.

*Makala hii imeandaliwa na mwandishi wetu kwa msaada wa mitandao mbalimbali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here