MKURUGENZI wa tafiti na uchapishaji Kituo cha Sera za Kimataifa-Afrika – Centre for International Policy-Africa (CIP-Africa) Thabiti Mlangi amesema asilimia 83 ya Watanzania waliohojiwa wamesema watashiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ili kuwachagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mlangi ametoa takwimu hizo leo, Oktoba 22, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa matokeo ya utafiti wa kura za maoni wa Taasisi hiyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo alisema, wamefanikiwa kuwahoji wananchi 1,976, wote wakiwa na sifa za kushiriki uchaguzi huo kwa kujiandikisha na kuwa na Vitambulisho vya Mpiga kura.
Aidha, ameeleza kuwa asilimia 53 ya wananchi hao wamekiri kushiriki kwenye Mikutano ya Kampeni za Vyama vya siasa, asilimia 76 kati yao wakihudhuria Mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), asilimia 15 wakihudhuria Mikutano ya ACT – Wazalendo, asilimia 7 wakihudhuria Mikutano ya Vyama vya siasa zaidi ya Kimoja na asilimia 2 wakihudhuria Mikutano ya Chama cha CHAUMMA.
“Kuhusu ushiriki katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Uraisi, ubunge na udiwani, asilimia 53 ya walioshiriki utafiti wameshiriki katika mikutano ya kampeni ya vyama vya siasa. Kati ya waliohudhuria kwenye mikutano ya kampeni, asilimia 76 walihudhuria mikutano ya kampeni ya CCM, asilimia 2 walishiriki mikutano ya kampeni ya CHAUMMA, asilimia 15 wameshiriki mikutano ya kampeni ya ACT-Wazalendo. Aidha, asilimia 7 wameshiriki katika mikutano ya kampeni ya chama zaidi ya kimoja,” amekaririwa Mlangi.
Mlangi amezungumzia pia masuala mbalimbali yaliyosemwa na wananchi ikiwemo matamanio yao ya kutaka mshindi wa nafasi ya urais kushughulikia changamoto za maji, miundombinu ya barabara na madaraja, uthibiti wa rushwa pamoja na usimamizi mkubwa wa huduma za elimu bora kwa wananchi.
Aidha, wengine pia wameonesha wasiwasi na hofu kwa wanafunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya hasa bangi, zaidi wananchi wa Ilala na Segerea wakitaka Rais ajaye ashughulikie jambo hilo kwa uzito.