SERIKALI imetangaza duru mpya ya utoaji wa Samia Scholarship kwa Mwaka 2026/27 kwa wanafunzi waliofaulu vizuri zaidi kwenye Masomo ya Sayansi katika mitihani ya kidato cha Sita.
Ufadhili huo unalenga kuandaa wataalamu wa kiwango cha Kimataifa katika fani za sayansi, teknolojia, uhandisi na Hisabati (STEM) , elimu tiba, Akili unde, Sayansi ya Data, Sayansi Shirikishi na Sayansi na teknolojia ya Nyuklia
Akizungumza Julai 27, 2026 jijini Dodoma na Waandishi wa habari Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa kundi la kwanza ni wanafunzi 1000 waliopata alama za juu katika tahasusi za sayansi wamechaguliwa kupata ufadhili huo.
Amesema kuwa masharti ya ufadhili kwa kundi hili ni Wanafunzi kujiunga na Vyuo Vikuu vya ndani katika Shahada za Hisabati, TEHAMA, Sayansi, Uhandisi na Tiba.
Mbali na kundi hilo, serikali pia imetangaza wanafunzi 50 bora zaidi waliopata ufaulu wa juu katika tahasusi za Physics, Chemistry na Mathematics (PCM), Physics, Mathematics na Computer Science (PMC) na Physics, Geography na Mathematics(PGM) ambao wameteuliwa kupata ufadhili wa Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+) Kusoma katika Vyuo Vikuu vinavyoongoza Duniani katika fani za Sayansi ya Data, Akili unde na Sayansi Shirikishi kwa Mwaka wa Masomo 2026/27.
“Wanafunzi hawa wataanza maandalizi kupitia kambi ya mafunzo (bootcamp) katika Taasisi ya Afrika ya Nelson ya Sayansi na Teknolojia (NM – AIST), Arusha,”amesema Prof. Mkenda
Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda ametangaza kuwa wanafunzi watatu wa Kitanzania wameteuliwa kupata ufadhili wa kusoma Shahada ya Uzamili ya Master of Technology (M. Tech) in Data Science and Artificial intelligence katika Taasisi ya Indian Insitute of Technology Madras (IITM) Kampasi ya Zanzibar
Aidha,Kwa wanafunzi 50 Waliokidhi vigezo vya kuomba Samia Scholarship Extended,majina yao yatapatikana kwenye tovuti ya Wizara www.moe.go.tz pamoja na ya NM-AIST www.nmaist.go.tz na wataomba ufadhili huo kupitia kiunganishi https://temis.moe.go.tz