‘Umeme wa REA umewafanya vijana wahamie vijijini’

0
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Jones Olotu, akizungumza na wahariri na waandishi wa habari (hawapo pichani) kueleza utekelezaji wa majukumu ya REA.

Na Mwandishi Wetu

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa REA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi Jones Olotu amesema moja ya mambo ambayo wanajivunia ni kubadilisha maisha ya vijana wengi wa vijijini ambao wamejiajiri na wengine waliokuwa mijini wamerudi vijijini kufuata fursa zinazopatikana kupitia nishati hiyo.

Mhandishi Olotu alizungumza hayo kwenye Kikao Kazi na Wahariri wa vyombo vya habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika kwenye ukumbi wa NSSF, Ilala kwa lengo la kuelezea utekelezaji wa majukumu ya REA.

Alisema, wakati REA inaanzishwa maeneo ya vijijini yaliyokuwa na umeme ilikuwa ni asilimia mbili, lakini hivi sasa sehemu kubwa imepata nishati hiyo na wanaendelea na jitihada za kufikisha umeme kwenye maeneo mengi zaidi.

Mhandisi Olotu alisema, Tanzania Bara kuna vijiji 12,318 ambapo hadi wakati anazungumza kwenye kikao hicho, vijiji 11,313 vimeunganishwa na umeme huku vijiji 1,005 vilivyosalia wakandarasi wapo kazini kukamilisha na kuwasha umeme, na kusisitiza ifikapo Juni 30, mwaka 2023 vijiji vyote 12,318 vitakuwa na umeme sambamba na kuimarisha njia za kusafirisha.

“Katika nchi za Sub – Saharan Afrika, Tanzania ni nchi ya kwanza kubadilisha equation ile ya vijana kuhama vijijini na kuhamia mijini kuja kutafuta fursa. Sasahivi vijana wanahama mijini wanakwenda vijijini kwasababu tumetengeneza fursa kule,” alisema Olotu.

Alisema, miaka ya nyuma kabla ya vijiji vingi kuwekwa umeme, iliwalazimu watu kutengeneza mjini bidhaa zinazohusisha chuma yakiwemo madirisha, milango au mageti na kisha kusafirisha kwenda vijijini kwasababu hakukuwa na huduma hizo, lakini hivi sasa kila kitu kinatengenezwa huko.

“Zamani ilikuwa chini ya mwembe unakuta wazee wamebandika kioo, kuna kiti na unakuta mzee anakunyoa na kiwembe, siku hizi hayo mambo hayapo tena, ukienda vijijini kuna saluni, watu wananyoa kwa kutumia umeme na vijana ndio ambao wanafanya hizo kazi,” alisema Olotu.

Aidha, aliongeza kuwa mbali na vijana kupata ajira, sekta za afya na elimu nazo zimepata ukombozi mkubwa, ambapo wameboresha hali ya utoaji wa huduma na wameunga takribani taasisi 42,000 ambazo zilikuwa hazina umeme hususani taasisi za afya, hivi sasa huduma za X Ray na MRI zinapatikana na akinamama wajawazito wanajifungua kwenye mazingira salama.

“Kuna wakati kabla ya umeme kufika vijijini, mjamzito anapokaribia kujifungua baba unaambiwa andaa kibatari, tochi, mafuta ya taa uje navyo, ikitokea usiku, tochi yako inamulika, mafuta unaweka kwenye kibatari ili wapate mwanga wa kumsaidia mama,” alisema.

Alisema, anakumbuka tukio ambalo lilitokea mwaka 2012, wakiwa Mbinga Mkoani Ruvuma, ambapo kulikuwa na mama mjamzito na mumewe wakiwa na kibatari kwa ajili ya kusubiri mama huyo ajifungue, ghafla wakawasha umeme kwa ajili ya majaribio, ikatokea taharuki kubwa ambapo mama huyo kwa mshtuko alijifungua.

“Wanakijiji wale waliona kama miujiza, wakauliza kilichotokea tukawaambia ni umeme wa Solar, wakataka kujua mengi kuhusu umeme huo, tukawaambia ni umeme wa jua, basi yule mtoto akapewa jina la Solar kutokana na tukio lile,” alisema Mhandisi Olotu, huku akiongeza kuwa, sekta ya elimu nayo imepata ukombozi, ambapo wanafunzi wanapata muda wa kujisomea hadi nyakati za usiku.

Mbali na usambazaji huo wa umeme vijijini, Mhandisi Olotu alisema, Serikali kupitia REA ipo mbioni kuhakikisha vitongoji 36,101 vinafikiwa na umeme, na tayari Serikali imeandaa mipango madhubuti na kufikia mwaka 2030 vitongoji vyote vitakuwa vimefikiwa na umeme.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage, alisema mbali na usambazaji wa umeme, REA ina jukumu la kuhakikisha wanapeleka huduma ya nishati mbadala kama mitungi ya gesi vijijini.

Alisema, kwa sasa wanatekeleza mradi wa usambazaji wa Mitungi ya Gesi ya Kupikia (LPG), kwenye maeneo mbalimbali nchini “Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 Jumla ya fedha takribani Shilingi Bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kusamabaza mitungi ya gesi ya kupikia na kwa sasa Wakala umeshatangaza kwa ajili ya wasambazaji wa mitungi kuomba.”

Mhandisi Advera alisema, mradi mwingine ni ule wa Kusambaza Gesi Asilia ya kupikia (CNG) katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na ambapo utekelezaji wake utahusisha REA na TPDC.

Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile akizungumza kwenye kikao hicho, aliipongeza REA kwa kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini, kwani hatua iliyofikia mpaka sasa ni kubwa na inayopaswa kuungwa mkono.

“Pongezi hizi siyo tu za kwenye jukwaa, kwa wale waliopata fursa ya kufika vijijini wakaona kinachoendelea hakuna sehemu utapita bila kuona nguzo imelala chini, hongereni sana kwa kazi mnayofanya, ” alisema Balile.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here