Ulega anadi fursa zinazopatikana Chato

0
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akimkabidhi mmoja wa washindi wa mbio za baiskeli katika Tamasha la Utalii " Chato Utalii Festival 2023" linalofanyika wilayani Chato, mkoani Geita Novemba 26, 2023.

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amefungua Tamasha la Utalii “Chato Utalii Festival 2023” linalofanyika wilayani Chato, mkoani Geita kwa lengo la kuhamasisha shughuli za utalii na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo mkoani humo.

Akizungumza wakati akifungua tamasha hilo Novemba 26, 2023 ambalo linaambatana na maonesho mbalimbali ya fursa zilizopo mkoani humo, alisema tamasha hilo limebeba dhana mbalimbali za uwekezaji hasa kwa upande wa kilimo, mifugo na uvuvi, utalii, utamaduni na michezo.

Alisema, fursa za uwekezaji zilizopo katika Wilaya ya Chato ni nyingi huku akiwahimiza wananchi na wawekezaji mbalimbali kuzitumia ili ziweze kuwaletea ufanisi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Aidha, Waziri Ulega alitumia fursa hiyo kutaja maeneo mbalimbali ambayo yana fursa za uwekezaji mkoani humo huku akibainisha kuwa katika sekta ya uvuvi pekee Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya Shilingi Bilioni 1.7 kwa ajili ya kujenga mwalo na soko kubwa la kisasa la samaki wilayani chato ambalo litatoa fursa za kibiashara na uongezaji thamani wa mazao ya samaki na dagaa.

Halikadhalika, aliongeza kwa kusema kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa takriban Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya kufanya  ujenzi wa kituo kikubwa cha  kuzalisha vifaranga vya samaki cha Rubambagwe kilichopo wilayani Chato ambacho kitawezesha wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika ukanda wa Ziwa Viktoria kuwa na uhakika wa kupata vifaranga bora vya samaki.

Kwa upande wa sekta ya mifugo, Waziri Ulega alisema Wizara imejenga mnada wa mifugo wa kisasa wa Buzirayombo ambao unatoa fursa kwa wafugaji kufanya biashara zao za mifugo kisasa huku akifafanua kuwa kufuatia uwepo wa idadi nzuri ya mifugo kunatoa fursa nyingine ya kujenga kiwanda cha kuchakata nyama.

Fursa nyingine alizozibainisha Waziri Ulega ni pamoja ujenzi wa hoteli kubwa za hadhi ya nyota tatu hadi tano kwa kuwa viwanja vinapatikana katika wilaya ya Chato, Kilimo cha umwagiliaji  kwa kuwa sehemu kubwa ya wilaya ya Chato imezungukwa na maji ya Ziwa Victoria na ujenzi wa viwanda vya Nguo kutokana na kuwepo kwa kinu cha kuchambulia pamba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here