Uholanzi waomba radhi kwa kushiriki biashara ya utumwa

0
Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte.

HAGUE, Uholanzi

WAZIRI Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte, ameomba radhi kwa niaba ya serikali ya nchi hiyo kutokana na taifa hilo kuhusika na biashara haramu ya utumwa huko nyuma.

Rutte alitoa tamko hilo katika kikao na waandishi wa habari mjini Hague mwanzoni mwa wiki, “Tunaweza kuutambua utumwa kwa njia ya wazi zaidi kama jinai dhidi ya binadamu.”

Bila kuashiria masuala ya fidia kwa familia za wahanga na waathiriwa wa utumwa, alisema Uholanzi inajuta na kusikitika kutokana na serikali ya nchi hiyo kwa karne kadhaa kuwezesha, kushajiisha na kustafidi na utumwa.

“Tunasikitika, dola la Udachi linabeba dhima ya madhila waliyoyapitia watumwa na vizazi vyao,” alisema Waziri Mkuu Uholanzi na kuongeza kuwa, nchi hiyo haipaswi kufumbia macho historia yake kama ya kuhusika na utumwa.

Nchi za Magharibi zimekuwa zikikwepa suala la kuwaomba radhi na kuwafidia wananchi wa nchi za Afrika kwa madhila na udhalilishaji waliofanyiwa katika enzi za utumwa.

“Afrika haiwezi kufikia maridhiano na Magharibi katika suala la utumwa, hadi pale Waafrika watakapoombwa radhi na nchi za Magharibi zilizonunua watumwa (wa Kiafrika), na kulilipa fidia bara la Afrika,” alisema Mustafa Mheta, mtafiti na Mkuu wa Dawati la Afrika la taasisi ya wanafikra ya Media Review Network yenye makao yake jijini Johannesburg alisema,

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, watu zaidi ya Milioni 50 kote duniani ni wahanga wa utumwa mamboleo, huku wanawake na wasichana miongoni mwao wakitumika kama watumwa wa ngono.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here