Tunafuata mfumo gani wa demokrasia?

0

Na Stanley Mayunga

SEPTEMBA 15 kila mwaka, tangu 2007 ni siku ya Kimataifa ya Demokrasia duniani baada ya kuidhinishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (????) ambapo inatoa fursa ya wadau kupitia hali ya demokrasia duniani.

Kuwepo kwa Serikali ya demokrasia kunatokana na majimbo ya kale ya mji wa Kigiriki karibu 500 B.C. Kwa zaidi ya miaka 2000, hata hivyo, demokrasia ilikuwepo mara chache na hasa katika maeneo yaliyotengwa

Kuongezeka polepole kwa demokrasia ya Kiingereza kisha Mapinduzi ya Marekani na Ufaransa mwishoni mwa karne ya 18 kulihitimisha mabadiliko ya demokrasia kutoka kuwa udadisi tu hadi wazo muhimu la Kisiasa la Kitaifa na Kimataifa.

Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, udikteta ulipitia wakati mgumu na waangalizi wengi walitangaza kuja kwa enzi ya Kidemokrasia.

Ilipendekezwa kwamba, tunaweza kuwa tumefika mwisho wa mageuzi ya kiitikadi ya wanadamu na kuenea kwa demokrasia huria ya Magharibi kama mfumo wa mwisho wa serikali.

Jinsi nchi zinavyotawaliwa ndani, kuna marekebisho kadhaa ya siasa za ulimwengu. Ili kuchunguza hilo hatuna budi kudadisi demokrasia.

Hata ikiwa haukubaliani na hoja kuhusu demokrasia ya mtindo wa Magharibi inayowakilisha mwisho wa mageuzi ya historia kisiasa, kuna shaka kidogo kwamba demokrasia imeenea kwa kiasi kikubwa katika miongo ya hivi karibuni na sasa ndiyo njia kuu ya utawala.

Suala hapa ni ikiwa mabadiliko haya ni mazuri, mabaya au hayana maana kuhusu siasa za ulimwengu. Lakini, bila kupinga faida za demokrasia, kuna mambo kadhaa magumu kuhusu juhudi za kuiuza (kuieneza) demokrasia. Ugumu huo unahusiana na vigezo kama; viwango vya demokrasia, uwezekano wa demokrasia na athari za demokrasia kwa usalama wa ndani.

Ugumu mmoja wa kukuza demokrasia ni kwamba, mara nyingi haiko wazi kuona nini ni kidemokrasia na nini sio!Lakini, tunaweza kujua hivyo kwa kuchunguza viwango kadhaa.

Jambo la muhimu ni kwamba, haki za mtu (ubinafsi) au ustawi wa jamii nzima (Ukomunisti). Wamarekani, Wakanada, Wazungu wa Magharibi na wengine wengi huwa wanasisitiza ubinafsi. Hii ni imani kwamba haki na uhuru wa mtu binafsi ni muhimu zaidi kwao.

Kinyume chake ni Ukomunisti unaodai ustawi wa pamoja lazima uthaminiwe kuliko faida za mtu yeyote. Viongozi wa nchi zenye uchumi duni mara nyingi wamesisitiza mapambano yao ya kulisha, kuvisha na vinginevyo katika kushughulikia mahitaji ya watu wao hayaruhusu ‘hanasa’ ya demokrasia ya mtindo wa Magharibi yenye mabishano ya kisiasa yasiyokoma na umakini wake kwa mtu binafsi (Individualism).

Kipimo kingine cha kupima kiwango cha demokrasia ni kati ya msisitizo wa mchakato hadi kuzingatia matokeo (Process – Outcome). Demokrasia ya kiutaratibu (Procedural Democracy) inasisitiza mchakato.

Ikiwa raia wana uhuru wa kusema, mara kwa mara na kuchagua miongoni mwa wagombea wanaoshindana na kufuata taratibu zingine kama hizo, basi kwa kiwango hiki kuna demokrasia.

Kutumia utaratibu kutathmini kiwango cha demokrasia ni dhahiri haswa katika dhana za Magharibi, lakini tamaduni zingine nyingi ulimwenguni zinasisitiza demokrasia kubwa (Substantive Democracy). Wao wanaiona demokrasia kama bidhaa muhimu inayohusishwa na usawa.

Wakosoaji wakubwa wa demokrasia ya kiutaratibu wanasema, nchi imeshindwa kidemokrasia ikiwa, licha ya kukidhi mahitaji yote ya kiutaratibu, inazalisha kiwango cha chini cha uchumi wa kijamii (kama ilivyo katika Amerika) kwa msingi wa rangi, kabila, jinsia au vigezo vingine.

Katika mfumo huo wanashindana. Ingawa wanapitia hoja zote za demokrasia, mwishowe wanakanusha jambo muhimu zaidi la kidemokrasia ambalo ni haki kubwa ya binadamu ya usawa.

Wakosoaji wanasema, mfumo wowote ulio na hali tofauti tofauti za kiuchumi asili yake sio ya kidemokrasia kwa sababu nadharia ya serikali ‘ya watu, na watu na kwa ajili ya watu’ inaendeshwa na uwezo wa watu matajiri, vikundi na Mashirika kutumia pesa nyingi kukodi washawishi wataalamu (Professional lobbyists), kulipia kampeni za uhusiano wa umma, kuchangia fedha za uchaguzi, kulipa mawakili kushtaki wapinzani kortini na vinginevyo kutumia misuli ya kiuchumi wanayokosa raia wengi. Hii inafanya ushindani kutokuwa wa haki wala kidemokrasia bila kujali nadharia yenyewe ikoje.

Katika demokrasia bora, kila mtu ambaye anataka kushiriki atakuwa na fursa sawa ya kufanya hivyo na kupanda hadi nafasi ya juu kabisa yaani ushawishi. Fursa hizo zingekuwepo kwa kweli, sio nadharia tu. Hakuna nchi ambayo imewahi kufikia ubora huo badala yake huwa kwenye kiwango fulani.

Upande mmoja, ushiriki wa maana ni mdogo sana; kwa upande mwingine ushiriki kama huo unagawanywa kwa upana kwa vigezo kama vile rangi, kabila na jinsia bila kujali mchakato wa kidemokrasia na matokeo.

Jinsia hutoa mwelekeo mzuri na muhimu kwa kuangalia kiwango hiki. Kwa kigezo hiki nchi nyingi bado ziko mbali kuelekea mwisho wa kipimo. Upigaji kura ilikuwa hatua muhimu kwa wanawake lakini ufikiaji wa ofisi za kisiasa umekuja polepole sana.

Mnamo 1893 New Zealand ilikuwa nchi ya kwanza kutambua haki ya wanawake kupiga kura. Mwaka 1902 Australia ikawa nchi ya kwanza kuwahakikishia wanawake haki ya kugombea uchaguzi, na wabunge wa kike wa kwanza waliochaguliwa duniani walichukua viti vyao katika bunge la Finland mnamo 1907.

Mwanamke wa kwanza isipokuwa mfalme kuwa mkuu wa nchi alikuwa Rais wa Presidium Yanjamaa Nemendeyen Sbaataryn wa Mongolia mnamo 1953, na Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke, Sirimavo Ratwatte Dias Bandaranaike wa Ceylon (sasa Sri Lanka) hakuingia madarakani hadi 1960.

Kuanzia hapo safu ya viongozi wa kisiasa wa kike imekua ingawa polepole. Kufikia mwishoni mwa 2003, ni wanawake 10 pekee walikuwa wakihudumu kama marais au Mawaziri Wakuu katika nchi zao.

Hakika, walikuwepo viongozi wanawake ambao wamejidhihirisha kuwa watetezi wa nchi zao wakati inahitajika. Kampeni ya kejeli kwamba wanawake hufanya viongozi dhaifu imekuwa ikikataliwa mara kwa mara na rekodi za viongozi wa kike kama vile WM Indira Gandhi wa India, WM Golda Meir wa Israeli, WM Margaret Thatcher wa Great Britain na kila mmoja akiiongoza nchi yake kushinda vita.

Vivyo hivyo, wanawake ambao wamehudumu safu ya maafisa wakuu wa uhusiano wa Kimataifa kama Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri wa Ulinzi pia wamethibitisha uwezo wao wakati inahitajika. Tunamkumbuka Madeleine Albright alipohudumu kama Katibu wa nchi wa Amerika kwa mafanikio.

Tanzania tumekuwa na mama zetu viongozi waliofanya kazi iliyotukuka na ambao wengine bahati mbaya rekodi zao zimesahaulika, lakini walau majina Bibi Titi, Getruda Mongella, Anna Abdallah, Anna Makinda si mapya katika siasa za Tanzania. Hivi sasa tunaye Rais wa JMT Mama Samia Suluhu Hassan ambaye awali alikuwa Makamu wa Rais.

Uzoefu na uhodari wake umetupitisha katika kipindi kigumu sana cha kuondokewa na aliyekuwa Rais wetu hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Hakika nchi imetulia na kazi zinaendelea. Hata hivyo, na yeye ameendelea kuwaamini wanawake na kuwajumuisha katika Serikali yake ili kutoa mchango wao katika kushiriki kulijenga Taifa letu.

Takwimu zinaonyesha wanawake katika nchi tofauti na wakati wa shida na mapito magumu wamekuwa na wastani mzuri wa hali ya kupambana kuliko wanaume wa nchi zao. Wachambuzi wengine wanaamini kuwa kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake kupitia mfumo wa kidemokrasia unaojumuisha (inclusive) kunaweza kupunguza mizozo ya ulimwengu kuliko mfumo dume au wa kuwatenga (Exclusiveness).

Uhusiano mwingine kati ya demokrasia na siasa za ulimwengu ni juhudi za kukuza demokrasia ulimwenguni. Hii inaibua maswala kadhaa. Moja, ni ikiwa demokrasia inawezekana mara zote angalau kwa muda mfupi.

Hivi karibuni sehemu zingine za ulimwengu tofauti na Magharibi zimeshuhudia kuongezeka kwa demokrasia, lakini uwezekano wa nchi yoyote moja kuchukua maadili yote na mazoea ya kidemokrasia inahusishwa walau na mambo ya ndani kama vile mitazamo kuhusu demokrasia na kiwango cha nchi cha elimu na uchumi.

Ni wazi kuwa, kuna uhusiano thabiti kati ya demokrasia na maendeleo ya uchumi. Kwamba, nchi za kidemokrasia zina pato la juu zaidi kwa kila mtu (Per Capita GDP) kuliko nchi zilizochanganya (demokrasia na mabavu) na nchi zile za mabavu pekee.

Pia, kujaribu kukuza demokrasia kamili katika nchi zenye hali mbaya ya kiuchumi na kielimu ni sawa na kujaribu kulazimisha mfumo wa kisiasa wa kigeni kwenye mfumo wa kijamii na uchumi ambao hauko tayari kwa hilo.

Kufanya hivyo kunaweza hata kudhibitisha kuwa hakuna tija. “Demokrasia tunayohimiza katika maeneo mengi masikini ya ulimwengu ni sehemu muhimu ya mabadiliko kuelekea aina mpya za ubabe” (Kaplan,1999:178) au kwa msemo mwingine ni kwamba “Demokrasia inaweza kuwa mbaya kwako”.

Hakika ni lazima tuijue tabia ya kitu demokrasia.Itakuwa kosa kudhani kwamba kila mtu,kila mahali anatamani kuwa huru, lakini karibu kila mtu, kila mahali anataka kuwa na uwezo wa kuikosoa serikali. Hii ni kwa mujibu wa uchunguzi.

Uchunguzi mwingine ulipouliza maoni ya watu juu ya kuwa na kiongozi hodari ambaye sio lazima ajisumbue na bunge au uchaguzi wengi waliafikiana na wazo hilo.

Uchunguzi mwingine ulilenga kupima vipaumbele kwa kuuliza wananchi nini wangependelea ikiwa wangechagua kati ya demokrasia na uchumi imara.Hapa napo wengi walichagua uchumi imara. Majibu kama haya yanasababisha kuhitimisha kuwa:-

“leo karibu kila mtu anatoa maoni; yaani anahoji kuhusu demokrasia…mmoja anapochunguza zaidi, mwingine hupata ushahidi unaomsumbua tu kwamba, msaada wa umma si wa kutegemewa.”

Kosa jingine kubwa itakuwa ni kudhani kwamba Marekani au nchi nyingine yoyote inaweza kufanikiwa kusafirisha mfano wa demokrasia yake kwa nchi zingine zote. Kwanza kabisa vipaumbele vinatofautiana.

Viwango vya Wamarekani, Waingereza na wengine huwa wanapendelea ubinafsi na demokrasia ya kiutaratibu. Wengine hawakubaliani na nadharia hizo bali zile za ukomunisti na Demokrasia kubwa.

Waamerika na Wafaransa waliulizwa ikiwa ni bora kwa serikali kuingilia kati jamii kidogo iwezekanavyo ili kuwaacha watu kutekeleza malengo yao au bora serikali ibebe jukumu kubwa katika jamii ili kuhakikisha kuwa hakuna raia mwenye uhitaji hatofikiwa.

Wamarekani wakahitaji kuachwa huru, lakini Wafaransa wakachagua kinyume chake yaani serikali inayojihusisha na jamii kwa kiasi kikubwa (Serikali ya kiharakati. Hapa tunapata nadharia ya demokrasia na maendeleo ya uchumi na kijamii; yaani watu wanavyohitaji kuishi katika nchi yao na kuwajibika bila kuvunja sheria.

Pamoja na maswala kadhaa hapo juu kuhusu uwezekano na hekima ya kukuza demokrasia, lakini juhudi hiyo pia ina athari muhimu kwa usalama wa ndani na wa Kimataifa.

Suala la demokrasia na usalama wa Kimataifa linazingatia mjadala wa muda mrefu juu ya ikiwa aina moja ya serikali imefanikiwa zaidi katika maswala ya kigeni hasa vita. Ni haswa katika mwenendo wa uhusiano wa kigeni kwamba, serikali za kidemokrasia zinaonekana kuwa duni kuliko serikali zinazotekelezwa kwa kanuni tofauti.

Kwamba, demokrasia huwa zinatii msukumo wa shauku badala ya maoni ya busara na pia m-demokrasia ana uwezo mdogo wa juhudi endelevu kuliko mwingine (asiye mdemokrasia). Itoshe kusema, demokrasia ni zaidi ya kuchaguana.

0621014417

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here