Tulinde, tuenzi utamaduni kwa manufaa ya vizazi vyetu – Majaliwa

0

▪️Asema tusikumbatie tamaduni zinazokwenda kinyume na maadili na ustaarabu

▪️Prof. Kabudi asema sarakasi ni mchezo unaongoza kuliingizia Taifa fedha za kigeni

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana wajibu wa pamoja wa kuhakikisha urithi wa utamaduni wa Taifa unalindwa, unaenziwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema hatuwezi kuwa na Taifa bila kuwa na utamaduni unaolitambulisha na kututofautisha na mataifa mengine.

“Utamaduni ni utambulisho wetu halisi kama Taifa. Utamaduni wa Taifa letu ndiyo unatufanya tutambuliwe kuwa sisi ni Watanzania bila kujadili tofauti za makabila, jamii au sehemu tunazotoka.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 22, 2025) alipofungua Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maendeleo ya Michezo kilichofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Kamwe tusikubali kukumbatia tamaduni zinazokwenda kinyume na maadili na ustaarabu wetu. Tusikubali kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni ambazo zinadhalilisha utu wetu. Pamoja na umuhimu wa kujifunza mambo mazuri ya tamaduni nyingine ni lazima kuchuja nini cha kuchukua na nini cha kuacha.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini sekta za utamaduni, sanaa na michezo kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa Taifa, hivyo wananchi washirikiane kuwarithisha watoto na vijana misingi ya utamaduni.

Aidha, Waziri Mkuu alisema pamoja na utambulisho wa jamii, kupitia sekta za utamaduni, sanaa na michezo, pia jamii inapata manufaa makubwa ikiwemo kuzalisha ajira kwa mamilioni ya Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa.

Majaliwa alisema, sekta hizo pamoja na kutumika kusukuma agenda mbalimbali za Kitaifa pia ni chanzo cha furaha, burudani, kuelimisha, kuonya na kuhamasisha umma katika nyanja mbalimbali.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzipa kipaumbele sekta za utamaduni, Sanaa na michezo na hivyo kuziwesha kuwa na mafanikio makubwa.

“Michezo ina nguvu na ushawishi mkubwa katika kuleta maendeleo na miongoni mwa michezo inayoongoza kuliletea Taifa fedha nyingi za kigeni ni riadha.”

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Mchezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta.

Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Hamisi Mwinjuma alisema ili kuendelea kuvutia mageuzi ya kidijitall, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, imefanikisha uunganishaji wa Mfumo wa Wadau wa Sanaa (AMIS) na Mfumo wa TAUSI.

Ametolea mfano mapato ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) yameongezeka kwa asilimia 200 kutokana na kuunganishwa kwa mifumo hiyo ya makusanyo.

Alisema, hatua hiyo si tu imeimarisha usimamizi wa sekta ya sanaa, bali pia imefungua ukurasa mpya wa uwazi, urahisi wa upatikanaji wa huduma, na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

“Kuanzia tarehe 26 Februari 2025, mifumo hii miwili inafanya kazi kwa pamoja, na sasa wadau katika maeneo 15 ya biashara – ikijumuisha studio za muziki, picha, video, huduma za burudani na ubunifu – wanaweza kupata vibali kwa njia moja ya haraka na ya wazi zaidi.”

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema, Kikao kazi hicho ni cha kimkakati katika kuleta mabadiliko makubwa kwa sekta za utamaduni, sanaa na michezo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita.

Alisema, kupitia vikao kazi vilivyopita, Wizara imewezesha kuanzishwa kwa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Kujengewa uwezo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usajili wa vyama na vilabu vya michezo nchini.

“Kupitia vikao hivi, tumeweza kuongeza idadi ya wataalamu wa utamaduni kutoka 43 mwaka 2021 mpaka 123 mwaka 2025 na Maafisa Maendeleo ya Michezo kutoka 48 mwaka 2021 hadi Maafisa Maendeleo ya Michezo 139 mwaka 2025.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here