Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amesema Serikali itatumia kiasi cha Shilingi Trilioni 2. 78 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu nchini
Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu, jijini Arusha .
Bashungwa alisema, kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) Serikali imetoa Shilingi Trilioni 1.2 lengo kwa la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya Sekondari, kuweka mazingira salama kwa wasichana waliopo katika shule za Sekondari, na kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza elimu ya Sekondari na kufikia malengo yao.
Bashungwa aliendelea kufafanua kuwa, Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST): Utatoa Shilingi Shilingi Trilioni 1.15. ambapo utaboresha mazingira ya kujifunzia katika shule za umma kwa kujenga miundombinu ya elimu, kuimarisha umahiri wa walimu na ubora wa ufundishaji darasani, kwa kutoa mafunzo endelevu ya walimu kazini.
Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo awamu ya Pili (EP4R II) utatoa Shilingi bilioni 435.90 kwa lengo la kuendelea kujenga miundombinu mbalimbali ya shule (madarasa, vyoo, mabweni, nyumba za walimu), pamoja na kununua vifaa vya kufundishia
Alieleza kuwa, afua zitakazotekelezwa ni pamoja Ujenzi wa Vyumba vya madarasa; Ujenzi wa Nyumba za Walimu; Ujenzi wa Maktaba; Ujenzi wa Matundu ya Vyoo; Ujenzi wa Mabweni; Ujenzi wa Mabwalo; Ujenzi wa Maabara; Ujenzi wa vyumba vya TEHAMA, Kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini, na Ununuzi wa Vifaa vya TEHAMA
Aidha, Waziri Bashungwa aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha wanafuatilia miradi yote ya Maendeleo ambayo fedha zake zipo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa inakamilishwa ifikapo Oktoba 31, 2022 na wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha miradi ya Maendeleo ifikapo tarehe hiyo taarifa itolewe ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.
Pia, aliwataka wakuu hao wa Mikoa kuhakikisha wanawasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ufanya matumizi sahihi ya fedha zote za miradi kwa kufuata Miongozo inayotolewa juu ya fedha hizo ili kupata thamani halisi ya fedha hizo kwa miradi inayotekelezwa
Bashungwa alielekeza kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo wanazoletewa ili kuepuka hoja za ukaguzi zisizo za lazima na kupata thamani ya fedha katika miradi hiyo.