TRA yazindua kampeni ya elimu ya kodi kwa biashara za mtandaoni

0

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Kampeni ya Elimu ya Kodi kwa Biashara za Mtandaoni kwa lengo la kuhakikisha kila anayehusika na biashara hizo anajisajili ili aanze kulipa Kodi.

Akizindua kampeni hiyo jana, Agosti 9, 2025, leo Jijini Dar es Salaam Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda amesema, wanaolengwa katika usajili huo ni Wafanyabiashara wenye kipato cha zaidi ya Shilingi Milioni 4 kwa mwaka ambao Kodi yao itakuwa Shilingi 100,000 kwa mwaka na kila mmoja atalipa kulingana na kipato chake.

Kamishna Mkuu Mwenda alisema, wakati wakiendelea kutoa Elimu kwa Wafanyabiashara wote wanaofanya biashara za mtandaoni kujisajili, wataanza na wanaofanya biashara ya kukodisha nyumba mtandaoni pamoja na wale wanaoendesha biashara mtandaoni ambao wamekuwa wakipata fedha nyingi na hawalipi Kodi.

Alisema, TRA itatoa asilimia 3 ya Kodi itakayookolewa kwa watu watakaotoa taarifa za ukwepaji wa Kodi kwa Wafanyabiashara watakaoshindwa kujisajili ndani ya muda uliowekwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wanaokwepa Kodi na watawatambua kwa kutokutoa risiti.

“Kila anayestahili kulipa Kodi atalipa kulingana na uwezo wake na mtaji wake na tupo kwaajili ya kuwezesha biashara hivyo hakuna mtu atakayeonewa katika utozaji wa Kodi,” alisema Mwenda.

Alisema, ili kuwezesha biashara wanaanzisha kitengo cha kuwezesha biashara katika kila mkoa wa Kodi kitakachosaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara na kutatua changamoto za Walipakodi ili kuwawezesha kulipa Kodi kwa hiari.

Kamishna Mkuu Mwenda alesema, ili kuhamasisha matumizi ya mtandaoni TRA imepunguza viwango vya VAT kutoka asilimia 18 mpaka 16 kwa Walipakodi watakaofanya malipo kupitia Mtandaoni na utekelezaji wa jambo hilo utaanza September Mosi mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana amesema hivi sasa mifumo ya BASATA inasomana na mifumo ya TRA Hali ambayo imerahisisha utoaji huduma na usajili wa wasanii na kazi za Sanaa na kurahisisha ulipaji wa Kodi kwa hiari.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) John Daffa alisema, wao ndiyo wasajili wa mitandaoni yote na Kampuni zinazoendesha shughuli za Mawasiliano nchini, hivyo watashirikiana na TRA kuhakikisha ulipaji Kodi kwa Biashara za Mtandaoni unafanikiwa.

Alisema, kila mtanzania anapaswa kuona fahari kulipa Kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here