Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imetangaza ukuaji mkubwa katika kipindi cha miaka mitano, huku idadi ya watumiaji wa bidhaa na huduma za bima ikiongezeka kutoka watu Milioni 5.6 mwaka 2021 hadi Milioni 26.8 mwaka 2025.
Mafanikio hayo yametangazwa na Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, kwenye mkutano wa wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu, Novemba 16, 2026.
Dkt. Saqware alisema, ukuaji huo umeambatana na ongezeko la mchango wa sekta ya bima katika Pato la Taifa (GDP) kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi asilimia 2.11 mwaka 2025.
Alisema, mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa usimamizi wa sekta ya bima, maboresho ya mifumo ya utoaji huduma, upanuzi wa wigo wa huduma pamoja na juhudi za kuongeza elimu ya bima kwa wananchi.
“Ongezeko la watumiaji wa huduma za bima limeenda sambamba na kuongezeka kwa kiwango cha wananchi wanaotumia na kunufaika na bima kutoka asilimia 8.9 mwaka 2021 hadi asilimia 39.3 mwaka 2025,” alisema,
Aidha, alisema wastani wa matumizi ya fedha kwa mtu mmoja kwa ajili ya bima umeongezeka kutoka Shilingi 15,334 mwaka 2021 hadi Shilingi 37,455 mwaka 2025s.
Alisema, katika kipindi hicho, thamani ya ada za bima zilizoandikishwa (Gross Written Premiums) imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 911 mwaka 2021 hadi Shilingi Trilioni 2.55 mwaka 2025.
“Pamoja na ongezeko hilo, thamani ya madai ya bima yaliyolipwa kwa mwaka imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 397.57 hadi Shilingi Trilioni 1.29 katika kipindi hicho,”
“Ukuaji huo pia umeonekana katika uwekezaji wa kampuni za bima, ambapo thamani ya mali zilizowekezwa imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 939.69 mwaka 2021 hadi Shilingi Trilioni 2.24 mwaka 2025,” alisema Dkt. Saqware.
Alisema, thamani ya mitaji katika soko la bima imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 416 hadi Shilingi Trilioni 1.89, huku uwezo wa sekta hiyo kuhimili vihatarishi ukifikia Shilingi Trilioni 193.53, sawa na asilimia 94.5 ya Pato la Taifa.
Dkt. Saqware alisema, ukuaji wa sekta ya bima umechangia pia kuongezeka kwa fursa za ajira, ambapo ajira rasmi zimeongezeka kutoka watu 3,737 mwaka 2021 hadi watu 15,398 mwaka 2025.
Wakati huohuo, Kamishna Saqware alisema, idadi ya watoa huduma za bima imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 10,940 mwaka 2025.
Pia, mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya Kidijitali ikiwamo TIRAMIS, ORS, TSS Portal, IRIS na E-Complaint kwa ajili ya kuboresha huduma za usimamizi, maombi ya leseni, uwasilishaji wa taarifa na kushughulikia malalamiko ya wateja.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kampuni za bima zinaendeshwa kwa misingi ya uwajibikaji, TIRA imeeleza kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya kifedha na kiutendaji ya kampuni za bima nchini.
Miongoni mwa viashiria vinavyoangaliwa kwa umakini ni upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi, malimbikizo ya madeni na madai ya wateja, kutokuwa na mikataba hai ya bima mtawanyo pamoja na upungufu wa amana ya dhamana inayotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania.
Viashiria vingine ni kutokuzingatiwa kwa misingi ya utawala bora, kutokufanyika kwa mikutano ya wanahisa na bodi pamoja na kuwepo kwa kesi nyingi mahakamani.
Dkt. Saqware alisema, hatua zinazochukuliwa dhidi ya changamoto hizo zinalenga kulinda maslahi ya wananchi wanaotumia huduma za bima na kuimarisha imani ya umma katika sekta hiyo.
Alisisitiza kuwa, kampuni za bima zinapaswa kuwa na mitaji toshelevu, kulipa madai ya wateja wanaostahili kwa wakati na kuhakikisha zinafuata sheria na kanuni zinazotawala biashara ya bima.
Katika eneo la bima ya afya, TIRA imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na Serikali katika kusimamia utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila gharama za matibabu kuwa kikwazo.
“Katika awamu ya kwanza Serikali ilihakiki na kuzipatia kadi za bima ya afya kaya 198,709 za wananchi wasio na uwezo wa kugharamia huduma hizo,” alisema Dkt. Saqware.
Aidha, katika awamu ya pili iliyozinduliwa Oktoba 22, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, Serikali inalenga kusajili kaya nyingine 625,000 za wananchi wasio na uwezo, sambamba na kupanua fursa kwa wananchi wenye uwezo wa kuchangia kujiunga na mfumo huo.
“Tunawahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi zilizosajiliwa na kuidhinishwa na mamlaka hiyo,” alisema Dkt. Saqware.
Kupitia mkutano huo, Saqware aliwataka wananchi kupata maelezo sahihi kuhusu vifurushi vya bima, huduma zinazogharamiwa, huduma zisizogharamiwa, masharti ya matumizi pamoja na utaratibu wa kuwasilisha malalamiko.
Mbali na ukuaji wa soko la bima, TIRA imeeleza kuwa nayo imepiga hatua katika utendaji wake wa ndani. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa gawio la taasisi kwa Serikali kutoka Shilingi Bilioni 3.56 mwaka 2021 hadi Shilingi Bilioni 5.13 mwaka 2025.
Pia, taasisi hiyo imeendelea kupata hati safi za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya 2022 hadi 2025.
Mafanikio mengine ni kukamilika kwa ujenzi wa makao makuu ya TIRA jijini Dodoma mwaka 2025, kuongezeka kwa mali za taasisi kutoka Shilingi Bilioni 11.18 hadi Shilingi Bilioni 21.72 na kuongezeka kwa watumishi kutoka 112 hadi 151 katika kipindi hicho.
Aidha, TIRA imeeleza kuwa imeongeza mtandao wa ofisi kutoka sita mwaka 2021 hadi 13 mwaka 2025, ikiwamo ofisi za kanda za Unguja na Pemba. “Katika tathmini ya utendaji wa mwaka 2024/2025 iliyofanywa kwa Bodi na Menejimenti ya TIRA, taasisi hiyo ilipata alama asilimia 86, zilizowekwa katika kundi la utendaji bora (Excellent).”