RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo, Novemba 16, 2026, amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa Ikulu, Dar es Salaam.
Kikao hicho kimejadili maoni ya wadau wa Baraza, uwakilishi wa vyama vya siasa na ushiriki wa wananchi kuelekea kuunda Tume ya Taifa ya Maridhiano.
Sambamba na hayo, Wajumbe hao pia wametoa maoni yao kuhusu mwelekeo wa mchakato wa Marekebisho ya Katiba, utakaotanguliwa na hatua ya Maridhiano.
Rais Dkt. Samia amesema vyama vya siasa vinatarajiwa kuwasilisha majina ya watu wawili kwa kuzingatia jinsia kwa kila chama, kwa ajili ya uteuzi wa Wajumbe wa Tume hiyo.
Ameongeza kuwa, baadhi ya majina ya wajumbe wanaopendekezwa tayari yamepokelewa, yakiwemo yaliyowasilishwa kutoka Zanzibar.
Kama sehemu ya uwakilishi, Rais Dkt. Samia amesema viongozi wa dini watapata nafasi ya kukutana na kutoa maoni yao kuhusu mchakato huo wa Maridhiano, akibainisha kuwa mashauriano hayo yataendelea wakati maandalizi ya kuunda Tume yakiendelea.
Aidha, ametoa wajibu kwa vyama vya siasa kusaidia kutoa elimu kwa wananchi ili wafahamu kazi ya Tume na jinsi ya kuwasilisha maoni yao pindi Tume hiyo itakapowafikia katika maeneo yao.
Akijibu swali la wajumbe kuhusu mchakato wa marekebisho ya Katiba, Rais Dkt. Samia amesema hatua inayokusudiwa ni kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo, akiongeza kuwa maoni ya wananchi yatasaidia kubainisha masuala mahsusi yanayohitaji mabadiliko.
“Yawe makubwa, yawe madogo, lakini ni marekebisho ya Katiba iliyopo,” amesema Rais Dkt. Samia, akibainisha kuwa Waraka wa Serikali kuhusu marekebisho hayo utaandaliwa baada ya kubainika kwa maeneo yanayohitaji mabadiliko.
Kwa upande wao, Baadhi ya wajumbe wamependekeza uteuzi wa wajumbe wa Tume uzingatie uwakilishi wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na ushiriki wa wanawake. Wengine wametoa maoni kuhusu uwakilishi wa vyama bila kujali ukubwa wake.
Wajumbe pia wamependekeza wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni kuhusu mwelekeo wa Katiba. Miongoni mwa mapendekezo mengine ni kusambaza kwa wananchi ripoti ya Kikosi Kazi kilichoshughulikia masuala ya demokrasia ya vyama vingi.
Kikao hicho kinaendeleza mashauriano ya Rais Dkt. Samia kuhusu maridhiano ya kisiasa. Katika vikao vya awali, Rais alikutana na wagombea urais na wagombea wenza wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.