MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amepongeza juhudi za uhifadhi zinazofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa Hifadhi ya Msitu wa Pugu–Kazimzumbwi umesaidia kulinda mazingira na rasilimali za taifa ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ujumbe wa Bodi ya Ushauri ya TFS ukiongozwa na Mjumbe wa Bodi, Piencia Kiure, Magoti alisema kuwa uwepo wa viongozi hao unathibitisha dhamira ya kweli ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za umma kwa maendeleo ya Taifa.
“Ugeni huu wa leo ni muhimu sana kwa sisi viongozi wa serikali. Unatupa nguvu, mshikamano, na unatekeleza kwa vitendo maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anataka taasisi zote za serikali kufanya kazi kwa kushirikiana,” alisema DC Magoti.
Piencia Kiure, kwa upande wake, aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano inaoutoa kwa TFS, na kusisitiza kuwa Bodi itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, hususan katika maeneo yenye umuhimu wa kiikolojia kama Kisarawe.
“Kwa niaba ya Bodi ya TFS, tunathibitisha kuwa tutaendelea kusimamia kwa karibu na kuimarisha juhudi za uhifadhi katika Wilaya hii ya Kisarawe na kwingineko nchini,” alisema Kiure.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo ya kikazi ya siku mbili kwenye Kanda ya Mashariki ya TFS, ujumbe wa Bodi umetembelea Hifadhi ya Vikindu pamoja na Pugu–Kazimzumbwi kwa ajili ya kukagua miradi ya uhifadhi na maendeleo inayoendeshwa ndani ya hifadhi hizo.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni ule wa Kuimarisha Ustahimilivu wa Bioanuwai ya Misitu ya Mazingira Asilia dhidi ya Matishio ya Mabadiliko ya Tabianchi, unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).
Kwa mujibu wa TFS, mradi huo unalenga kuboresha huduma za kiikolojia, kuimarisha maisha ya wananchi wanaozunguka hifadhi na kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika uchumi wa Taifa.
Ziara hiyo inaendelea kesho ambapo wajumbe wa Bodi wanatarajiwa kukutana na watendaji wa TFS Kanda ya Mashariki na kutembelea maeneo mengine ya kimkakati kwa ajili ya tathmini na ushauri wa kitaalamu.