Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kutoa wito kwa wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia ili kulinda misitu na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Juni 3, 2025 na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alipotembelea mabanda mballimbali katika maonesho yanayofanyika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.
Maonesho hayo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yenye kaulimbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”
Akizungumza na wanahabari, Prof. Silayo alisema misitu ni nguzo kuu ya mfumo wa ikolojia, na kwamba mazingira hayawezi kulindwa ipasavyo pasipo uhifadhi wa misitu.
“Mazingira yanapoharibika, fikra huenda moja kwa moja kwa miti iliyokatwa na misitu iliyopotea. Hii inaonyesha kwa kiasi gani misitu ni moyo wa mazingira yetu,” alisema Prof. Silayo.
Aliongeza kuwa uharibifu wa misitu una madhara makubwa katika sekta zingine ikiwemo maji, kilimo, mifugo na afya ya jamii.
Katika hotuba yake, Prof. Silayo alipongeza maafisa na askari wa TFS kwa kutoa elimu kwa wananchi kupitia maonesho hayo, akisema elimu hiyo inaendana na juhudi za kitaifa za ulinzi wa misitu, utunzaji wa mbegu bora za miti, upandaji wa miche, na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
“Ninaona elimu inatolewa kwa kiwango kizuri sana – kuanzia mbegu, miche hadi faida za kiikolojia. TFS mmejipanga vizuri, hongereni sana,” alisema.
Prof. Silayo alisema, TFS itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi, iliyozinduliwa Juni 2, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko.
Lengo la mkakati huo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za nishati safi na kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.
“Tunahitaji kuwasaidia wananchi waelewe umuhimu wa kuachana na mkaa na kuni. Elimu hii lazima itolewe kwa nguvu zote,” alisisitiza.
Akihitimisha, Prof. Silayo alitoa wito kwa wananchi na taasisi mbalimbali kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo pamoja na kampeni za mabadiliko ya tabia kuhusu matumizi ya nishati.
“Taasisi zote zishirikiane nasi kutoa elimu kwa umma, kama Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyosisitiza. Tusiwaache wananchi nyuma,” alisema.
Alisema, utegemezi wa nishati ya mimea, hasa kuni na mkaa, bado ni tishio kwa uhai wa misitu, hivyo hatua madhubuti zinahitajika ili kubadili mwelekeo huo.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni 5, kwa lengo la kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kulinda mazingira. Maonesho ya mwaka huu jijini Dodoma yamehusisha taasisi za Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na wananchi kwa ujumla katika juhudi za pamoja za kuhifadhi mazingira, kupunguza matumizi ya plastiki na kukuza matumizi ya nishati safi.