Teknolojia mbadala inavyochangia kasi ya TARURA kufikia malengo yake

0

Na Iddy Mkwama

LICHA ya Serikali kuongeza bajeti kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), lakini bado kuna upungufu wa fedha ambao unasababisha kujitokeza kwa changamoto wakati wa utekelezaji wa majukumu ya wakala huo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TARURA, bajeti kwa mwaka 2021/22 hadi 2024/25 imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 25.431 hadi Shilingi Bilioni 52.334 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 205.79.

Hata hivyo, katika kukabiliana na changamoto hiyo ya upungufu wa fedha, TARURA imeamua kutumia teknolojia ya ujenzi wa mawe kwa ajili ya kujenga barabara na madaraja ambayo yanasaidia kuokoa fedha nyingi.

“Tukisema tutegemee bajeti yetu kwa ujenzi wa zamani wa nondo na zege, itachukua miaka mingi, tukaamua kutumia vifaa vya ujenzi vinavyopatikana kwenye maeneo yetu,” anasema Mhandisi Pharels Ngeleja, Msimamizi wa Teknolojia Mbadala, TARURA kwenye semina na waandishi wa habari wa jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Pharels Ngeleja, Msimamizi wa Teknolojia Mbadala, TARURA

Mhandisi Ngeleja anasema, teknolojia hiyo imekuwa nafuu na inasaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu, ikizingatiwa inatumia vifaa vinavyopatikana kwenye maeneo husika.

Anasema, kwasasa wanaendelea na kasi kubwa ya ujenzi, ambapo kwa nchi nzima tangu mwaka 2017, yamejengwa madaraja 401 na yanasaidia huduma mbalimbali za kijamii, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi kwenye maeneo yalipojengwa.

“Ukiwa na daraja, hata kama barabara ni mbovu, unafika unapopataka. Kuna wagonjwa wanataka kwenda kupata huduma za afya, kuna wakulima wanataka kusafirisha mazao yao, kuna wanafunzi wanataka kwenda shule, waumini wanaokwenda kuswali na kusali, kwahiyo, daraja ni kiungo cha kwanza ili tuweze kuendelea; madaraja ni namba moja,” anasema.

Aliendelea kusema, “Kwa mfano, unakuta barabara nzuri, lakini pale pamejaa maji, utapitaje? Hauwezi kupita bila kuwa na daraja. Kwasababu hiyo sasa, ili tuweze kujenga miundombinu mingi, madaraja mengi, sisi TARURA tumeamua kutumia mawe, kujenga madaraja ya mawe.”

Mhandisi Ngeleja anasema, mbali na kusaidia kuinua uchumi na kuwasaidia wananchi kufika wanapokwenda kwa haraka, madaraja ya mawe yanadumu kwa miaka mingi.

“Madaraja la mawe ni imara na yanakaa muda mrefu na yanapunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 80 na unaweza kupita vile vile kama unavyopita kwenye madaraja yanayojengwa kwa zege,” anasema kuwaondoa wasiwasi watu wanaoamini kwamba, magari yenye mzigo wa tani nyingi hayawezi kupita kwenye madaraja hayo.

Aidha, Mhandisi Ngeleja anasema, ujenzi kwa kutumia mawe, unapunguza uharibifu wa mazingira, kwani hauna haja ya kuwa na mitambo mingi kama inavyofanyika wakati wa ujenzi kwa kutumia zege.

“Kwenye ujenzi mkubwa wa daraja, kuna mitambo; itakuwa inatoa moshi, unaharibu mazingira. Hapa ni kukusanya mawe na kwenda kuyajengea moja kwa moja, kwahiyo uharibifu wa mazingira ni mdogo,” anasema.

Mhandisi Ngeleja anasema, ujenzi wa aina hii haupo Tanzania pekee, bali upo kwenye nchi mbalimbali kwa miaka mingi tangu karne ya 14. “China wanatumia ujenzi huu.”

Pia, reli yetu ya kati kwenda Kigoma, madaraja mengi yamejengwa kwa mawe, chukulia treni inayobeba mizigo inapita, lakini hayo madaraja hadi leo yapo na yanaendelea kutumika.”

Anasema, kuna nchi za Ulaya ambazo zina madaraja yaliyojengwa miaka 200 au 300 iliyopita, “kwahiyo madaraja haya, ukiacha ni gharama nafuu, yanaishi karne, sisi TARURA kipindi hiki tumeona tuyajenge ili yaishi vizazi na vizazi.”

Mhandisi Ngeleja anasema, mpaka sasa kuanzia mwaka 2017/2018 wana madaraja 401 na wameokoa kiasi kikubwa cha fedha baada ya kuanza kutumia teknolojia hiyo.

Alitolea mfano wa daraja lililopo Wilaya ya Mkalama, (Msingi Stone arch bridge), ambapo awali walipofanya usanifu, ilitakiwa watumie Shilingi Bilioni 1.3, lakini walipoamua kutumia mawe, walitumia Shilingi Milioni 300.72, “lipo na linatumika kwa magari yote.”

Anasema, daraja hilo limekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo, kwani walikuwa wanazunguka Kilomita 25 kwenda kwenye soko kuu la Nyakitonto, lakini baada ya kukamilika, wanatembea umbali wa Kilomita 12. “Huko wana miradi mingi ya umwagiliaji, wanalima mpunga.”

Mhandisi Ngeleja anasema, kukamilika kwa daraja hilo kumewainua wananchi hao kiuchumi na kuwapunguzia gharama za usafirishaji wa mazao, ambapo awali kusafirisha Kilo 100 kabla ilikuwa Shilingi 1000, lakini hivisasa wanalipa Shilingi 500.

Aidha, kabla ya ujenzi wa daraja hilo, magari yalikuwa hayafiki, na idadi ya baiskeli na pikipiki ambazo zinabeba mazao zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kwenye eneo hilo muhimu lenye mazao mbalimbali.

Akizungumzia faida zaidi za ujenzi wa kutumia mawe Mhandisi Ngeleja anasema, umetoa ajira kwa wananchi wengi ambapo watu zaidi ya 10,000 wamenufaika kwa kufanya shughuli za ukusanyaji wa mawe na wengine mamantilie ambao wamekuwa wakitoa huduma kwenye maeneo ya miradi.

“Pia, kama tunavyopiga kelele kila kuhusu wizi wa vifaa kwenye miradi, huku suala hilo halipo maana hauwezi kuiba jiwe. Ni teknolojia ambayo imedhibiti wizi kwa kiasi kikubwa sana. Vile vile, haihitaji eneo kubwa la kuhifadhi magari na mitambo inayohusika kwenye ujenzi,” anasema.

Anasema, Kigoma ndio mkoa ambao unaongoza kwa kuwa na madaraja mengi ya mawe, ambapo yapo 155 na mengine yanaendelea kujengwa. “Tulipata ufadhili, mfadhili akawa anatoa fedha, misumari na vifaa vingine, wananchi wakawa wanakusanya mawe,”

“Wananchi wa Kigoma walijitoa sana, halmashauri zilijitoa kuhamasisha wananchi, TARURA tulijitoa kusimamia ubora wa kazi hadi tukafikia hapo.”

“Ni mikoa michache sana ukiwaambia wananchi wajitoe wakafanya hivyo, nawapongeza wananchi wa Kigoma kwa kujitoa mpaka mradi unafungwa, tulikuwa na madaraja 110. Tumejenga na wananchi wa Kigoma kwa kujitolea.”

Aidha, kwa mkoa wa Iringa, anasema wao wamejenga madaraja kwa kutumia matofali ya kuchoma ambayo yamethibitishwa ubora wake kabla ya kutumika kwenye ujenzi “madaraja haya yote tumejenga kwa kutumia Bilioni 23, lakini tungejenga kwa zege tungetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 91.”

Kupitia semina hiyo, Mhandisi Ngeleja alitoa taarifa ya uwepo wa daraja moja la mawe ambalo limejengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, huku wakitarajia kujenga daraja jingine la Mita 80, kwenye Mto Mzinga.

Mbali na ujenzi wa madaraja ya mawe, Mhandisi huyo anasema, wanaendelea na ujenzi wa barabara za mawe kwenye mitaa ya mikoa takribani minne na tayari wamejenga Kilomita 28.92 na wametumia Shilingi Bilioni 10, ambapo kama wangetumia lami nyepesi, zingetumika zaidi ya Shilingi Bilioni 16, lami nzito zaidi ya Shilingi Bilioni 42.

“Zamani wale wanaoishi Mwanza, kwenda Hospitali ya Bugando ukitokea Igogo, ilikuwa ni lazima uzungukie Nata, sasahivi tumejenga barabara ya mawe kutoka Igogo, pale Toyota unanyoosha hadi Bugando,” anasema.

Kutokana na ujenzi wa barabara hiyo, wananchi wengi wanafika kwa wakati kupata huduma za afya, “huenda kuna watu walikuwa wanafariki kwasababu ya kuzunguka Nata, hatuna data kamili ya tumeokoa maisha ya wangapi, ila nina uhakika wapo.”

Mbali na Mwanza anasema Ujiji, Kigoma kwa Dkt. Livingstone, imejengwa barabara ya mawe na ujenzi kwenye maeneo mengine unaendelea.

“Barabara hizi zinasaidia kudhibiti mwendo kasi wa magari, kwasababu ukiingia unalazimika kwenda polepole, spidi ni 40 kwa saa na watu wanapita,” anasema na kuongeza kuwa, ujenzi huo umewasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa fedha sambamba na kupunguza gharama za ukarabati.

Anasema, barabara ambazo zimejengwa kwa kutumia lami, likipatikana shimo, gharama ya kwenda kuziba shimo moja ni kubwa; kwasababu linahusisha mitambo mingi.

“Kwenye viraka vyote vya lami, ni lazima ubebe mitambo yote, ni gharama sana, kwenye barabara ya mawe, unaenda na kibarua mmoja na toroli la mchanga, unatoa lile jiwe unaangalia shida unarudishia mchanga na unarudisha jiwe, pia zinakaa miaka 100 hadi kufanyiwa matengenezo,” anasema.

Vile vile anasema, kwenye barabara za lami wanazuia watu wasimwage Oil za magari kwasababu ya athari zinazojitokeza, lakini kwenye barabara ya mawe hakuna athari yoyote.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Geofrey Mkinga anasema, mbali na kuendelea na majaribio ya teknolojia hiyo ya ujenzi wa kutumia mawe, wanaendelea na utafiti wa teknolojia nyingine.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Geofrey Mkinga

“Katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na Wakala tunaendelea kufanya majaribo kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja ya mawe (Stone arch bridges) pamoja na teknolojia nyingine ili kuboresha barabara tunazosimamia,” anasema Mkinga.

Aliendelea kusema: “Wakala unaendelea na utafiti wa teknolojia mbadala za Ecoroads, Ecozyme na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira.”

Mhandisi Mkinga anasema, Wakala umeimarisha upatikanaji wa miundombinu ya barabara za Wilaya zenye urefu wa Kilomita 5,057.765 kwa asilimia 55 Kitaifa na asilimia 52 Kimkoa, huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 60 ifikapo Juni, mwaka huu.

Wakala wa TARURA wenye jukumu la kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za Mijini na vijijini, ulianzishwa Mei 2017 na unasimamia Kilomita 144,429.77, ambapo lengo liliwekwa hadi kufika mwaka huu 2025, asilimia 85 ya barabara za Wilaya ziwe zinapitika kwa misimu yote.

Ni wazi kwa kasi na mipango inayoendelea kutekelezwa, lengo hilo litafikiwa na kuhakisi kauli mbiu yao inayosema “TARURA tunakufungulia barabara kufika kusipofikika.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here