Na Hassan Kimweri, Addis Ababa
TANZANIA imesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwekezaji katika sekta ya afya ili kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma kwa wananchi, wakati wa mawasilisho na majadiliano kwenye kikao cha pembezoni mwa Mkutano wa 76 wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, unaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Mawasilisho hayo yametolewa Agosti 26, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa ambapo katika wasilisho kuhusu Mkakati wa Ufadhili wa Afya kwa Mustakabali wa Sekta ya Afya kwa Kanda ya Afrika kwa mwaka 2026–2035, Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha ufadhili wa ndani, kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali na kupunguza gharama za huduma zinazolipwa moja kwa moja na wananchi.
Aidha, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto kuanzia kipindi cha ujauzito hadi kufikia umri wa miaka minane huku mkazo ukiwekwa kwenye kuimarisha afya, lishe, elimu ya awali, malezi yenye mwitikio pamoja na ulinzi na usalama wa watoto.
Kuhusu eneo la udhibiti wa bidhaa za afya, Tanzania imeweka bayana hatua iliyofikia kwa kiwango cha tatu cha ukomavu wa mfumo wa udhibiti, huku ikiendelea na juhudi za kufikia kiwango cha nne sambamba na Nchi wanachama kutakiwa kutenga rasilimali za kutosha na kuimarisha ushirikiano katika eneo hilo.
Kuhusu mapambano dhidi ya malaria, Tanzania imeeleza hatua inazochukua kukabiliana na changamoto zinazojitokeza, zikiwemo kuongezeka kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu, mabadiliko ya mifumo ya maambukizi pamoja na changamoto za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya huduma za malaria.
Wasilisho na majadiliano hayo yameweka bayana msisitizo katika kuharakisha upatikanaji wa bidhaa na teknolojia bunifu za afya, dawa salama na zenye ubora, pamoja na kuimarisha mifumo ya uzalishaji na udhibiti wa bidhaa za afya zinazokidhi viwango.
Hatua hizo zinatarajiwa kuchangia kuboresha huduma za afya kwa Watanzania, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote na uzalishaji wa bidhaa za afya zenye kukidhi viwango vya ubora ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye gharama nafuu.
Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania uliwakilishwa na viongozi kutoka Wizara ya Afya, akiwemo Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Razalo Mihiga, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dkt. Felix Bundala, pamoja na Mkuu wa Sekretarieti ya Rasilimali za Sekta ya Afya, Dkt. Vivian Wonanji.