SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zinatarajia kutekeleza wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa uvuvi wa bahari utakaofanyika kwa mwaka mmoja na nusu hadi Januari 2028.
Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Prof. Mohammed Sheikh mbali na kuahidi ushirikiano kwenye utekelezaji wa mradi huo amewataka wavuvi watakaoshiriki kwenye utekelezaji huo kuainisha yale wanayohitaji yaguswe na mradi huo.
“Kumekuwa na athari kubwa sana katika sekta ya Uvuvi kuanza kuharibika kwa matumbawe na hata joto la maji na ardhini limekuwa kubwa mpaka upatikanaji wa samaki umepungua hivyo tunaamini mradi huu utakuja kushughulikia na eneo muhimu sana kwa wavuvi,” amesema Prof. Sheikh.
Kwa upande wake mwakilishi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ambaye pia ni Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Salim Ahmed Hamza amesema, mradi huo una manufaa makubwa kwa wavuvi waliopo visiwani Zanzibar ambapo pia utaunga mkono juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tulikuwa tunafanya mradi unaitwa “Inuka na uchumi wa buluu” kupitia fedha zilizokuwa chini ya mfuko wa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 na moja ya changamoto zilizoonekana wakati huo ni maeneo yaliyokuwa ya wakulima wa mwani na wavuvi waliokuwa wakivua karibu na pwani kuathiriwa na mabadiliko ya tabia hivyo Serikali ilitoa takribani boti 500 kwa lengo la kuwapeleka mbali zaidi ili waondokane na changamoto hiyo,” ameongeza Hamza.