Na Francis Godwin, MUFINDI
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Water for Africa limetajwa kuwa miongoni mwa wadau muhimu wanaosaidia Serikali katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mufindi, hususan Jimbo la Mufindi Kusini, kupitia uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza katika jukwaa la Mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) lililofanyika Kata ya Mbalamaziwa, Tarafa ya Malangali Katibu wa mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini Aida Kaduma amesema, Water for Africa imekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia wananchi kupata huduma ya maji safi na salama kwa kuchimba visima katika vijiji, shule, vituo vya afya na maeneo ya makazi.
Amesema kabla ya shirika hilo kuongeza nguvu katika eneo hilo, baadhi ya wananchi walikabiliwa na changamoto kubwa ya maji, huku maeneo kama Kata ya Ihowanza yakikumbwa na ukame na ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya maji, hali ambayo kwa sasa imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na uchimbaji wa visima.
“Tunaishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu na kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, akisema Serikali haiwezi kufanya kila kitu peke yake hivyo ushirikiano na wadau ni muhimu katika kuharakisha maendeleo,” amesema.
Aidha, amesema kuwa Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kienzile, amekuwa akishirikiana na mashirika hayo kwa kuyaelekeza katika maeneo yenye changamoto ya maji, huku akitoa pongezi kwa Water for Africa kwa kuitikia mahitaji ya wananchi na kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Meneja wa Water for Africa Tanzania, Nestory sanga, amesema shirika hilo ambalo ni lisilo la kiserikali limekuwa likitekeleza miradi ya maji katika hospitali, shule, vijiji na maeneo mengine yenye changamoto ya maji, huku akieleza kuwa juhudi hizo zinalenga kusaidia Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Sisi Water for Africa tumejikita kusaidia wanakijiji kuondokana na adha ya maji, tunahakikisha wananchi wanapata maji kwa urahisi na kwa gharama nafuu, tumepeleka maji, mashuleni, hospitalini na maeneo mengine ambayo yanawawezesha wananchi kupata huduma ya maji,” amesema.