📌 Kukamilika kwa barabara hiyo kuchochea uchumi wa Kanda ya Afrika Mashariki
UJENZI wa barabara ya Lusahunga–Rusumo yenye urefu wa Kilomita 92 umefikia asilimia 69, huku Serikali ikieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea usafirishaji wa watu na bidhaa na kuongeza shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Barabara hiyo ni sehemu muhimu ya mtandao wa barabara wa Afrika Mashariki unaoiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Emmanuel Luchemba kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Kagera, amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kati ya Tanzania na nchi hizo.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaimarisha shughuli za uzalishaji, hususan katika sekta za kilimo, biashara, usafirishaji na uchimbaji wa madini, kwa kuwezesha mazao, bidhaa na rasilimali nyingine kusafirishwa kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Luchemba, mradi huo pia utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha upatikanaji wa masoko ya ndani na ya kikanda.
Kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Serikali inaijenga upya kwa kiwango cha lami kinachoweza kuhimili magari mazito, huku ikitumia usanifu wa kisasa wa tabaka la lami unaojulikana kama Superpave.
Amesema matumizi ya usanifu huo yanalenga kuongeza uimara wa barabara, kupunguza gharama za matengenezo na kuimarisha usalama wa watumiaji.
Mhandisi Luchemba amesema mradi huo ulianza Julai 5, 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 10, 2026. Unatekelezwa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kutoka China, huku huduma za ushauri wa uhandisi zikitolewa na Kampuni ya NORPLAN Tanzania Limited kwa ubia na TYPSA.
“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa chini ya Programu ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP), inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuongeza ufanisi wa mtandao wa barabara nchini,” amesema Mhandisi Luchemba.