KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Deodatus Mwanyika, imepokea taarifa za utekelezaji wa majukumu kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika kikao kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.
Katika taarifa yake, Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) imeeleza kuwa biashara ya nyama nje ya nchi imeendelea kuimarika, ambapo Tanzania imeingiza Dola za Marekani Milioni 61.5 kutokana na mauzo ya nyama katika nchi 11.
Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 8.4, ikilinganishwa na mwaka uliotangulia huku, Nyama ya mbuzi imeongoza kwa kuchangia asilimia 67 ya jumla ya nyama yote iliyouzwa nje ya nchi.
Kwa mwaka 2025/2026, jumla ya tani 14,213.66 za nyama zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 61.5 ziliuzwa nje ya nchi, ikilinganishwa na tani 13,112.44 zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 53.9 mwaka 2024/2025.
Kwa upande wa tasnia ya maziwa, taarifa imeeleza kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka lita bilioni 3.9 mwaka 2023/2024 hadi kufikia lita bilioni 4.2 mwaka 2025/2026, kiwango hicho ni sawa na asilimia 97 ya lengo la kuzalisha lita bilioni 4.3 za maziwa kwa mwaka.
Tasnia hiyo pia inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wananchi, ambapo inagusa takribani kaya Milioni 4.6 na kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa zaidi ya Watanzania Milioni 20.
Baada ya kupokea taarifaa hizo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Deodatus Mwanyika aliongoza waongoza wajumbe kujadili taarifa hizo ambapo pamoja na maoni na ushauri walioutoa kwa wizara na taasisi zake wajumbe pia walipongeza utekelezaji wa majukumu unaofanywa na taasisi hizo na kutoa maagio kuhusu namna bora ya kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi.