TANZANIA imefanikiwa kushuhudia utiaji saini wa mikataba na hati tatu za makubaliano za kimkakati zenye lengo la kukuza uchumi, kuboresha nishati, na kuimarisha sekta ya afya nchini.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alisema hayo wakati akizungumza na vyombo vya Habari baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM) pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Infra for Africa Forum), uliofanyika tarehe 5 na 6 Agosti, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam.
Alisema kupitia jukwaa hilo la siku mbili lililofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, likiwakutanisha wadau mbalimbali wa kimataifa ikiwemo taasisi za fedha za maendeleo na wawekezaji wa sekta binafsi limekuwa na mafanikio kwa Tanzania kufuatia kusainiwa kwa hati hizo tatu.
‘‘Tumesaini hati ya makubaliano katika sekta ya afya ya kujenga kituo kipya cha huduma za usafishaji wa figo (dialysis) ambapo mradi huu unalenga kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, hususan yale yanayohusiana na matatizo ya figo, kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za dialysis’’, alisema Balozi Omar.
Alisema, hati ya pili iliyosainiwa ni ya mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa gesi kimiminika akibainisha kuwa mradi huo mdogo wa viwanda unalenga kurahisisha matumizi ya gesi katika kuendesha viwanda vya ndani kwa haraka wakati mijadala ya mradi mkubwa wa gesi ikiendelea.
Balozi Omar alisema, hati ya tatu iliyosainiwa ilihusu makubaliano kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Africa50 kuhusu ushirikiano katika kuendeleza miundombinu ya usafirishaji wa umeme.
‘‘Jukwaa la Miundombinu lilitupatia nafasi ya kujadili kwa kina mustakabali wa maendeleo ya miundombinu barani Afrika ambapo katika mjadala wa kufunga wataalamu walisisitiza kuwa kutokana na mabadiliko ya kisiasa duniani, Afrika inapaswa kuimarisha uwezo wake wa kujitegemea na kuimarisha ajenda zake za maendeleo,’’ aliongeza Balozi Omar.
Mikutano hiyo iliyobeba Kauli mbiu ya “Miaka kumi ya mafanikio kutoka maono hadi utekelezaji – A Decade of Economic Impact: From Ambition to Delivery”, imeipatia Tanzania fursa ya kutangaza vivutio vya utalii, uwekezaji na miradi ya kimkakati kwa lengo la kuvutia mitaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu.