WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo ya vijijini, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za mafuta na kuchochea maendeleo ya shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Akizungumza na wadau waliotembelea Banda la REA katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Advera Mwijage alisema, mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za nishati na kuongeza fursa za maendeleo vijijini.
Alisema sambamba na mradi wa vituo vidogo vya mafuta, REA inaendelea kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu na teknolojia mbadala kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata nishati salama, nafuu na endelevu.
Mwijage alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utachangia kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji, kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi, pamoja na kuharakisha ukuaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini.
Aidha, aliwahamasisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea Banda la REA katika Maonesho ya Nane Nane ili kupata elimu kuhusu miradi inayotekelezwa na wakala huo pamoja na fursa zinazopatikana katika sekta ya nishati vijijini.
Miradi hiyo inaendana na jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa wote na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia maendeleo ya uchumi wa vijijini na matumizi ya nishati endelevu.