RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kipimo cha uongozi barani Afrika si idadi ya matamko, bali ni matokeo yanayoboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza Agosti 5, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu kwa Afrika jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema maendeleo hupimwa kwa uwepo wa miundombinu yenye tija kama barabara, reli, nishati, bandari na mifumo ya kidijitali inayochochea ajira na uwekezaji.
“Ni wazi kwamba wananchi wetu hawapimi maendeleo kwa kauli au ahadi tunazotoa, bali kwa matokeo yanayoonekana kama vile barabara, nishati ya uhakika, bandari na reli zenye ufanisi, miundombinu ya kidijitali, pamoja na miundombinu inayozalisha ajira, kuvutia uwekezaji na kuboresha maisha ya watu,” amesema.
Amesema Tanzania imeendelea kujijengea imani kama kitovu cha uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.