TANZANIA imeendelea kuthibitisha utayari wake wa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Ufugaji Nyuki (Apimondia) mwaka 2027 baada ya wajumbe wa Baraza Kuu la Apimondia na Kamati ya Maandalizi ya Kitaifa kutembelea kituo cha kipekee cha ufugaji nyuki wasiuma, kijulikanacho kama BEEtopia, kilichopo Meru, Arusha.
Kituo cha BEEtopia, kilichoanzishwa na Warren Steyn, kimekuwa mfano wa ubunifu wa Tanzania katika kukuza utalii wa nyuki na uhifadhi wa mazingira.
Kikiwa pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, kituo hiki kimejipatia umaarufu kama kivutio adimu kinachotoa elimu kuhusu nyuki wasiouma, rasilimali ambayo mara nyingi hupuuzwa kutokana na umaarufu wa wanyama wakubwa wa porini nchini.
“Tanzania ina takribani spishi 12 za nyuki wasiouma na nne kati ya hizo zinapatikana hapa BEEtopia,” alisema Steyn. “Dhamira yetu si asali pekee, bali ni uhifadhi, utafiti, elimu na kusaidia jamii zetu kuvuna asali bila kuharibu makundiya nyuki porini. Tunataka wageni waondoke hapa wakiwashukuru viumbe hawa wadogo wanaosaidia maisha ya viumbe wakubwa kuendelea kuwepo.”
Kupitia mtandao wa wafugaji nyuki wa maeneo ya Kilimanjaro na Mlima Meru, BEEtopia huwafundisha wakulima mbinu endelevu za kugawa makundi ya nyuki, kufungasha asali kwa ajili ya masoko ya ndani na ya kimataifa, na kuwaelimisha watalii kuhusu umuhimu wa nyuki katika uchavushaji na uhifadhi wa bioanuwai.
Timoth Mdinka, Mkurugenzi Mtendaji wa Learning and Discovery Africa (LAND Africa) na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Apimondia 2027, alisema ufugaji nyuki una mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii nchini.
“Kanda ya Kaskazini ndiyo kitovu cha utalii wa Tanzania,” alisema Mdinka. “Tunaendelea kuwaambia makampuni ya safari: ‘Fikirieni nyuki, fikirieni nyuki.’ Utalii wa nyuki unaleta ladha mpya, mtalii anaweza kuanza na nyuki kabla ya kwenda Serengeti au Kilimanjaro. Hii inawafanya wageni wakae Arusha kwa muda mrefu zaidi na kunufaisha jamii kwa upana.”
Mdinka alibainisha kuwa tayari kuna ratiba mpya za utalii wa nyuki zinazoundwa ili wageni wabaki katika kanda hii kwa angalau siku mbili zaidi, hatua ambayo itachangia kukuza biashara ndogondogo na uchumi wa wananchi wa maeneo ya jirani.
Rais wa Kamisheniya Afrika ya Apimondia, David Mukomana, alisifu uongozi wa Tanzania katika tafiti za nyuki wasiouma. “Kuna pendekezo la kuanzishwa kwa kikundi kazi cha kimataifa kuhusu nyuki hawa, kitakachounganisha Asia, Afrika na Amerika ya Kusini. Maarifa yanayokusanywa hapa BEEtopia yatakuwa ya msaada mkubwa kwenye juhudi hizo,” alisema Mukomana.
Mukomana pia aliwaalika wataalamu wa Tanzania kushiriki vikao vya Apimondia vitakavyofanyika Copenhagen mwaka huu, ambako mwongozo maalum utakaoonyesha vivutio vya utalii wa nyuki vya Tanzania utawasilishwa,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa polisi Benedict Wakulyamba, alihakikishia wajumbe wa Apimondia kuwa Serikali ipo tayari kikamilifu kuhakikisha kongamano hilo linafanyika kwa mafanikio.
“Serikali imejipanga kuhakikisha Apimondia 2027 inakuwa kongamano la kipekee, si kwa Tanzania pekee bali kwa bara zima la Afrika,” alisema Wakulyamba. “Mbali na vivutio vyetu vikubwa, tuna hazina nyingine ambazo hazijulikani sana kama nyuki wasiouma. Tutasimama bega kwa bega na wadau wote kuhakikisha mafanikio ya tukio hili.”
Ujumbe ulipokamilisha ziara yao, Steyn alihitimisha akisema: “Utalii wa nyuki unalenga kufungua macho ya watu kutambua kazi kubwa inayofanywa na hawa nyuki wadogoo wanaolinda mifumo ya ikolojia. Tukifanya vizuri, Tanzania haitakuwa mwenyeji wa Apimondia pekee bali tutaendelea kuuvutia ulimwengu.”
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema kuwa kupitia BEEtopia na mtandao wa wadau wa ndani, safari ya Tanzania kuelekea Apimondia 2027 ina kila dalili za mafanikio.