Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA imeishukuru Taasisi ya Trademark Afrika (TMA) kwa mchango wao katika kuboresha mifumo mbalimbali inayochangia kuimarika kwa mazingira ya biashara uwekezaji nchini.
Shukrani hizo zimetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa inayosimamia utekelezaji wa miradi ya TMA nchini (National Oversight Committee -NOC), Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati akifungua Mkutano wa Pamoja wa Wenyeviti wa NOC, Bodi ya Wakurugenzi wa TMA na Washirika wa Maendeleo wa TradeMark Afrika (TMA).
Dkt. Mwamba alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023, Serikali imeshuhudia mageuzi makubwa ya kimifumo na kiutendaji kufuatia kukamilika kwa baadhi ya miradi ikiwemo mradi wa kusimika skana ya kupimia mizigo katika mpaka wa Tunduma, mradi wa mfumo wa kutoa vibali vya uwekezaji, na mfumo wa kutoa vibali kwa wafanyabiashara wa mifugo na bidhaa za mifugo, ambayo imeongeza ufanisi wa utoaji huduma.
Alisema, kusimikwa kwa mfumo wa skana katika mpaka wa Tunduma, kumepunguza muda wa upimaji na uondoshaji mizigo kutoka wastani wa siku 5 hadi siku moja huku mradi wa dirisha moja la kielekroniki la uwekezaji umepunguza muda wa kupata vibali kwa wawekezaji na kupunguza gharama za kupata vibali vya uwekezaji nchini.
Dkt. Mwamba aliyataja mafanikio mengine yanayotokana na uwekezaji wa Trademark Afrika kuwa ni kuimarika kwa upatikanaji wa masoko ya bidhaa za mbogamboga na maua kwa kuwaunganisha na masoko ya uhakika wakulima 964 ambao waliuza kilo milioni 2.1 zenye thamani za zaidi ya shilingi bilioni 3.6.
“Pia Trademark Africa, wameiwezesha Tanzania kupitia Taasisi ya TMX, kwa kujenga mfumo wa kimtandao unaowawezesha wakulima kuuza mazao yao ya kilimo na mifugo kwa faida kupitia mfumo huo na kuwawezesha wakulima kupata faida na Serikali kukusanya ruzuku” alisema Dkt. Mwamba
Dkt. Mwamba alisema, Tanzania imepitia upya na imeboresha mifumo yake ya kodi hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji na kutoa wito kwa wajumbe wa Mkutano huo, kuimarisha ushirikiano hususan katika eneo la kukuza biashara na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuinua biashara, uchumi na maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Program ya Trademark Africa, Allen Asiimwe, alisema katika muongo mmoja uliopita, TMA imewekeza kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 1.2 ikiwa ni jitihada za kuboresha uzalishaji, kuimarisha biashara na mazingira ya uwekezaji katika nchi wanachama.
Alisema kuwa jitihada hizo pamoja na za nchi wanachama bado jitihada kubwa zinahitajika kwa nchi wanachama kuboresha uuzaji wa bidhaa nje pamoja na kuimarisha mifumo ya kidigitali inayoweza kuchochea biashara na uwekezaji.
Aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kwamba TMA itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu kwa nchi wanachama wake ambapo kwa Tanzania, pamoja na miradi mingine, Taasisi hiyo inatarajia kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza zaidi ufanisi wa Bandari hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi na ukanda mzima wa maziwa makuu.
Asiimwe alizungumzia pia umuhimu wa kukuza biashara kwa njia ya mtandao ambayo imeendelea kukua kwa kasi na kuwavutia vijana wengi zaidi wanaojipatia kipato kupitia njia hiyo jambo ambalo linaweza kuongeza mapato ya Serikali na kukuza pia kiwango cha ajira.