Tanzania na Vietnam kuendeleza ushirikiano

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Ho Duc Phoc, mazungumzo yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Jijini Sevilla, nchini Hispania.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania inathamini ushirikiano ulipo baina yake na Vietnam ambao umedumu kwa miaka 60 hivi sasa.

Alisema, Vietnam ni kati ya nchi za kwanza zilizofungua ubalozi mapema zaidi mara baada ya uhuru na kushirikiana na Tanzania kupitia Serikali, Chama Cha Mapinduzi na Wananchi.

Alisema, Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano mzuri uliopo na Vietnam ikiwemo kuunga mkono kwenye masuala yenye maslahi ya pamoja katika majukwaa ya kimataifa.

Makamu wa Rais alisema, ushirikiano uliopo baina ya Tanznia na Vietnam unapswa kuongezwa zaidi katika uwekezaji, kilimo, biashara masuala ya ulinzi na kushirikiana pia katika masuala ya Kikanda na Kimataifa.

Ameishukuru Serikali ya Vietnam kwa kuridhia soko la bidhaa mbalimbali za Tanzania kama vile Korosho na bidhaa za misitu.

Makamu wa Rais ameipongeza Vietnam kwa kuandaa Tume ya Kwanza ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC) mwaka 2014 na kuihakikishia kwamba Tanzania itaandaa Tume ya Pili ya Pamoja ya Ushirikiano mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ameikaribisha Vietnam kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania kama vile kilimo, viwanda vya nguo pamoja na viwanda vingine vya uzalishaji.

Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na inatatua changamoto zote zinazojitokeza katika uwekezaji kupitia majukwaa mbalimbali ya utoaji maoni yaliyoandaliwa.

Alisema, Serikali ipo tayari kushirikiana Kampuni ya Vietnam ya Viettel inayomiliki Mtandao wa Simu wa Halotel kuendelea kufikisha huduma bora ya mtandao ikiwemo 5G.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam Ho Duc Phoc alisema, Tanzania na Vietnam ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Vietnam katika majukwaa ya Kimataifa na hivyo kudumisha ushirikiano mzuri uliopo.

Alisema, ushirikiano wa kiuchumi unaendelea kuimarika ambapo Tanzania inatumia soko la Vietnam kuuza Korosho na bidhaa za misitu na kila mwaka mauzo ya biashara hizo hufikia Dola Milioni 150.

Alisema, uchumi wa Mataifa hayo mawili unaendelea kutegemeana kwa kuwa Vietnam inazalisha bidhaa ambazo zinauzwa nchini Tanzania ikiwemo mavazi na chakula.

Ameongeza kwamba ni vema kuendelea kuimarisha ushirikiano zaidi kwa kuwa bado yapo maeneo ambayo yanaweza kuwekezwa zaidi kupitia mashirika mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji ya Vietnam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here