Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania itaendelea kutoa mchango wake katika Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ili kuwezesha utekelezaji mbalimbali wa miradi unaofanywa na mfuko huo.
Dkt. Mpango alisema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Dkt. Geraldine Mukeshimana, Ikulu Jijini Dar es Salaam, ambapo aliweka wazi kwamba, mageuzi katika sekta ya kilimo ni kipaumbele cha serikali ya Tanzania kwa kuwa inatambua umuhimu wake katika uchumi wa nchi.
Makamu wa Rais alitoa wito kwa IFAD kuona umuhimu wa kuongeza eneo la mradi wa urejelezaji ardhi katika maeneo yanayokabiliwa na ukame Tanzania bara na Zanzibar. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji kulingana na uwekezaji halisi wa miradi ili iweze kutekelezwa kwa wakati.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa IFAD kushirikiana na Tanzania katika tafiti za kina zitakazowezesha matumizi ya ardhi katika maeneo yenye ukame husasani maeneo ya kanda ya kati ya nchi ili iweze kutumika katika kilimo.
Pia, alisema ni muhimu kuweka mkazo katika miradi itakayowezesha matumizi sahihi ya rasilimali za majini kama vile baharini na katika maziwa ili kwenda sambamba na vipaumbele vya nchi katika sekta ya uchumi wa buluu.
Kwa Upande wake Makamu wa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Geraldine Mukeshimana alisema, Tanzania imekuwa ni mdau muhimu katika mfuko huo kwa kuwa mchangiaji mzuri na hivyo kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Dkt. Mpango alisema, kutokana na athari za migogoro ya kimataifa na uviko 19 iliyosababisha ukosefu wa chakula katika maeneo mengi, IFAD inalenga kuhamasisha uchangiaji wa rasilimali fedha kutoka kwa nchi washirika ili iweze kutoa mchango wake katika kuimarisha sekta ya kilimo.