Na Shaban Juma, Dar es Salaam
NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Denmark katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha huduma za afya, kuongeza upatikanaji wa matibabu bora na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi.
Dkt. Samizi amesema hayo leo Juni 05, 2026 wakati akimwakilisha Waziri wa Afya katika maadhimisho ya miaka 177 ya Siku ya Katiba ya Denmark, ambapo ameeleza kuwa Denmark imeendelea kuwa mshirika wa muda mrefu wa Tanzania katika maendeleo ya sekta ya afya kwa miongo takribani sita.
Amesema kupitia programu ya kusaidia sekta ya afya (Health Sector Programme Support), Denmark imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za afya nchini, kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu pamoja na kusaidia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika utoaji wa huduma za afya.
Dkt. Samizi amesema taasisi mbalimbali ikiwemo Christian Social Services Commission (CSSC), CCBRT, APHFTA, Marie Stopes Tanzania pamoja na Sikika zimefanikiwa kunufaika na ushirikiano huo, hatua iliyosaidia kuboresha matokeo ya afya kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini.
“Uwekezaji huu haujaimarisha taasisi pekee bali pia umeokoa maisha, kulinda familia na kupanua fursa za wananchi kuishi maisha yenye afya bora,” amesema Dkt. Samizi.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kufurahishwa na ushirikiano unaoendelea kupitia mpango wa Danish Strategic Sector Cooperation, ambao utaendelea kuimarisha mahusiano ya sekta ya afya kati ya Tanzania na Denmark.
Katika hotuba yake, Dkt. Samizi pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha diplomasia ya afya na ushirikiano wa Kimataifa unaochochea maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Aidha, ametuma salamu za pongezi kwa wananchi wa Denmark katika maadhimisho ya miaka 177 ya Siku ya Katiba yao huku akisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na Taifa hilo katika kuimarisha afya na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.