Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, kwasasa kinasubiri maamuzi ya Kamati za bunge na vikao vya wabunge wa chama hicho (party Caucus) kisha watamuita na kumuhoji mbunge wa Tunguu, Zanzibar Simai Mohamed Said.
Hivi karibuni, mbunge huyo alitoa tuhuma nzito dhidi ya mtu ambaye hakumtaja jina, lakini alidai anaihujumu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Simai alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia bajeti ya Wizara ta Fedha, ambapo alidai ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuba ‘Yuda’.
Kauli hiyo, imezua mjadala mkubwa, ambapo kumezuka tafsiri mbalimbali, huku wapo wanaodai Simai ametumwa na kundi linalojipanga kwa mbio za Urais 2030, na wengine wakimtaja mmoja wa viongozi kama ndiye aliyelengwa na mbunge huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema, ni vema kwasasa watanzania wakasubiri maamuzi ya bunge, kisha chama kitafuata taratibu zake.
Mbeto alisema, CCM ina vikao vyake vinavyohusisha wabunge wote, hadi sasa hakijakaa, vile vile bunge nalo lina Kamati zake, nalo halijatoa taarifa yoyote, hivyo maamuzi yakishafanyika, chama nacho kupitia utaratibu wake kitamuita Simai na kumuhoji.
“Sisi kama chama, Simai angetamka nje ya bunge, tungechukua hatua moja kwa moja, mbunge anapoongea jambo akiwa ndani ya bunge anakuwa na kinga zake, kuna mambo ya maadili wenyewe wanajua, bunge litamuita, maana tuhuma alizozitoa ni nzito,” alisema Mbeto.
Akifafanua zaidi alisema, Simai amedai kuna wasaliti, chama kitataka kujua ni akina nani ambao wanamsaliti Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na huo ndio utaratibu ambao utatumika na bunge na chama ambacho mbunge husika anakiwalisha bungeni.
“CCM ndio iliyokwenda kuomba kura kwa Watanzania, CCM ndio iliyokwenda kuomba kura kwa Wazanzibar na ikachaguliwa, kukamkabidhi Rais Samia, akatafuta wakumsaidia, sasa kama kuna mtu amepewa dhamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hafanyi vizuri au anamuhujumu, lazima chama tujue,” alisema Mbeto.
Aliongeza kuwa, CCM kina utaratibu wake; kina Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa na vikao vya maadili, hivyo hana shaka kwamba yaliyosemwa chama kina taarifa zake, na hata Rais ana taarifa kupitia kwa vyombo vyake mbalimbali.
“Rais ni taasisi, si mtu kama mnavyomuona Samia, tusubiri kanuni za bunge na maadili. Niseme tu, alilosema nimelisikia, limetuhuzunisha,” alisema Mbeto na kusisitiza kuwa, anaamini yote aliyoyasema Simai ni kutokana na utashi wake binafsi kwasababu anazozijua mwenyewe, hivyo haamini kama nyuma yake kuna mtu yeyote.