Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa amesema, idadi ya Wanyama adimu imeongezeka kwenye hifadhi mbalimbali nchini.
Alisema hayo leo Novemba 10, 2026 katika mkutano wa wahariri na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, na kufafanua kuwa, hiyo ni moja ya viashiria muhimu vya mafanikio ya uhifadhi.
“Moja ya vipimo vya mafanikio ya hifadhi ni kuongezeka kwa baadhi ya wanyama adimu ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira na shughuli za kibinadamu,” alisema.
Aliendelea kusema, idadi ya faru imeongezeka kutoka 128 mwaka 2021 hadi kukadiriwa kufikia 170 mwaka 2026. Vilevile, sokwe wameongezeka kutoka 196 hadi 288 katika kipindi hicho.
“Katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, TANAPA imeendelea na juhudi za kuzalisha na kurejesha mbwa mwitu katika mazingira yao ya asili, ambapo mbwa mwitu 12 wapo katika eneo la uzalishaji huku wengine 25 wakiwa wameachiwa kwenda kwenye maeneo yao ya asili,” alisema Kamishna Mwishawa.
Aidha, alisema mafanikio haya yanaonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ulinzi, tafiti na usimamizi wa makazi ya wanyamapori ili kuhakikisha urithi huo unaendelea kupatikana kwa vizazi vijavyo.
Mbali na kuongezeka kwa Wanyama hao adimu, Kamishna Mwishawa alisema alisema katika eneo la uhifadhi wa mazingira, TANAPA imefanikiwa kudhibiti mimea vamizi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 9,440.22 ndani ya hifadhi 15 za taifa.
‘Pia, hekta 1,546 zilizokuwa zimeathirika na uwepo wa vichaka zimesafishwa ili kurejesha hali ya mazingira na kuboresha makazi ya wanyamapori,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, hatua nyingine ni kurejeshwa kwa shoroba ya Katavi-Mahale kwa kuondoa shughuli zilizokuwa zinahatarisha kuziba kwa njia muhimu zinazotumiwa na wanyamapori, hususan tembo na sokwe.
Aidha, TANAPA imeimarisha ulinzi wa makazi ya sokwe katika Hifadhi za Taifa za Gombe, Milima ya Mahale na Kisiwa cha Rubondo.
Katika kukabiliana na ukame alisema, Shirika limechimba visima virefu vinane, kujenga mabwawa sita, kusafisha mabwawa 19 na kuondoa vizuizi katika mifereji saba ya vyanzo vya maji. Pia, limefanya ufukuaji wa mchanga kwenye mabwawa 36 katika Hifadhi ya Taifa Ruaha.
“Hatua hizo zina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha wanyamapori wanapata maji hata wakati wa kiangazi, huku zikisaidia kulinda uwiano wa mifumo ikolojia,” alisisitiza Kamishna Mwishawa.