JUMUIYA ya Wataalamu wa Kiislamu (Tanzania Muslim Professionals Association – TAMPRO) imefanikiwa kutoa mikopo inayogharimu Shilingi Bilioni 13 kwa wanachama wake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.
Taasisi hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1997, inalenga kuwawezesha Waislamu na Jamii kwa ujumla ili kuboresha maisha yao katika nyanja mbalimbali za Kimaisha.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi unapofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa TAMPRO, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Haji Mrisho alisema, pamoja na kutoa mikop hiyo, bado wanaendelea kutafuta njia za kuhakikisha wanaiwezesha zaidi jamii Kiuchumi.
“Tumefanikiwa kutoa mikopo kwa wanachama wetu kupitia TAMPRO SACCOS na bado tunaendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwawezesha wanachama wengi zaidi,” alisema Mrisho.
Alisema, katika kutafuta namna ya kufikia malengo hayo, Mkutano wa mwaka huu pamoja na mambo mengine, utajadili changamoto za ajira na kutafuta mbinu za kukabiliana na jambo hilo, kutafuta uwezo wa kuwasaidia Kiuchumi vijana na akinamama, na pia watajadili namna ya kuijengea uwezo Taasisi hiyo.
“Hivi sasa mbali na Serikali, sekta binafsi nayo inatoa ajira, kwa hiyo tutajadili namna ya kutengeneza fursa za ajira na kutafuta njia za kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wakuze biashara zao, vile vile tutajadili namna ya kuiongezea Taasisi yetu nguvu ya Kiuchumi,” alisema.
Kwa upande wake Mgeni Maalum kwenye Mkutano huo, Balozi Mstaafu Dkt. Ramadhan Dau alisema, miongoni mwa mambo ambayo yanakwamisha maendeleo ya Taasisi nyingi hapa nchini, ni kukosa uwezo wa Kiuchumi.
Dkt. Dau alishauri Taasisi hizo ikiwemo TAMPRO, zitafute namna ya kuanzisha vitega uchumi, na watafute watendaji ambao watabuni miradi na kuisimamia.
“Tufanye uwekezaji, tuajiri watalaamu wa kusimamia mipango yote ya Kiuchumi ili Taasisi zijiendeshe, tunaweza kufanikiwa zaidi kwenye hilo iwapo tutajipanga vizuri,” alisema Dkt. Dau.
Naye, Prof. Mussa Assad ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano huo aliipongeza TAMPRO – SACCOS kwa kufanikiwa kutoa mikopo kwa wanachama wake, ingawa alisema bado jitihada zaidi za kuwawezesha wanachama zinahitajika.
“Ni SACCOS ya muda mrefu sana na imestahimili, nimeisikia fedha ambazo zimetolewa kuwakopesha wanachama, ni hatua kubwa sana ila bado jitihada zaidi zinahitajika ili kuwafikia wengi zaidi,” alisema Prof. Assad.
Aidha, Prof. Assad kupitia Mkutano huo, alipendekeza baadhi ya miradi ambayo inaweza kuanzishwa ili kujenga uchumi imara wa Taasisi hiyo inayojumuisha wanataaluma kutoka mikoa mbalimbali nchini.