Taasisi za Umma zatakiwa kutumia Maonesho ya Sabasaba kujitangaza

0

Na Mwandishi Wetu

OFISI ya Msajili wa Hazina imetoa rai kwa taasisi za umma kutumia maonesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba kama jukwaa la kutangaza huduma zinazotolewa na Serikali.

Akizungumza Jumatatu, Julai 1, 2025, katika viwanja vya Sabasaba, Sabato Kosuri ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema wananchi ndio wamiliki wa taasisi za umma na hivyo wanahaki ya kujua uwekezaji uliofanyika.

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imewekeza kiasi cha Shilingi Trilioni 86.25 katika taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.

Kati ya kiasi hicho Shilingi Trilioni 83.33 zimewekezwa kwenye taasisi 152 ambazo Serikali ina hisa nyingi, huku Shilingi Trilioni 2.82 zikiwekezwa kwenye kampuni 56 ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.

Kosuri alisema, Maonesho ya biashara ya Sabasaba ni mwendelezo wa tafsiri ya ndoto ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuongeza ufanisi wa taasisi za umma lengo likiwa ni kuleta tija na rejesho halisi la uwekezaji uliofanywa katika taasisi za umma.

“Sisi kama wasaidizi wa Mhe. Rais tumedhamiria kutengeneza mazingira ya uwajibikaji kwani taasisi za umma ni mali za umma na hivyo zinawajibika moja kwa moja kwa umma,” alisema.

Kosuri alisema, ushiriki wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na taasisi inazozisimamia katika maonesho ya Sabasaba utawapa fursa kwa wadau na wananchi kwa ujumla kuuliza maswali na kutoa maoni.

“Tutumie maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kupokea maoni na kuwaambia wadau na wananchi kwa ujumla mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayafanya,” alisema Kosuri.

Alihitimisha kwa kuwakaribisha wadau mbalimbali na wananchi wote katika banda namba 39 la Ofisi ya Msajili wa Hazina lililopo katika ukumbi wa Kilimanjaro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here