SMZ yaahidi kuimarisha ustawi wa Vijana

0

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema kuwa Serikali, ikitambua mchango na umuhimu wa vijana, inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha ustawi na maendeleo yao kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hemed ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari Utaani, Wete – Pemba.

Alisema, lengo la maadhimisho hayo ni kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa, pamoja na kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto zao ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Hemed alieleza kuwa, Serikali imeimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za maendeleo ya vijana kwa kusambaza na kujenga uelewa wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2023 kwa wadau mbalimbali, na kwa sasa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inaandaa toleo la lugha nyepesi ili liwe rahisi kueleweka na vijana wengi zaidi.

Aidha, alisema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 16.5 kwa ajili ya miradi ya vijana, ikiwemo uwekezaji katika vituo vya maendeleo na kusaidia miradi ya kiuchumi kupitia mabaraza ya vijana.

Katika kuwawezesha vijana kiuchumi, Serikali inaendelea kuimarisha mfuko wa mikopo ya vijana kupitia mfumo wa 4.4.2, ambapo sasa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umeweka mfumo wa maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao.

Akizungumzia ajira, Hemed alisema Serikali imeanzisha mradi wa SEBEP kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta ya uchumi wa buluu kupitia vituo vya amali.

Ili kufanikisha hilo, Serikali itajenga vituo vingine saba vya amali na kuandaa mtaala maalum wa ajira katika uchumi wa buluu utakaotumika kufundishia.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kukarabati viwanja vya zamani na kujenga vipya katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, ili kukuza sekta ya michezo na kutoa fursa zaidi kwa vijana kushiriki.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alisema Siku ya Vijana Duniani ni fursa kwa vijana kujitathmini, kushughulikia changamoto zao na kujipanga kwa mafanikio.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here