WATANZANIA wamekumbushwa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki kwani athari zake ni kubwa kwa afya ya binadamu na viumbe hai na mazingira kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji alipotembelea na mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea kwenye Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Dkt. Kijaji alisema kuwa mifuko ya plastiki isipodhibitiwa ikitupwa ovyo na kuingia kwenye vyanzo vya maji vikiwemo bahari na maziwa ina athari kubwa kwa samaki na mazalia yake pindi.
“Sote tutambue mifuko hii si salama kwa maisha yetu pamoja na mifugo na samaki, kwa mfano inapoingia baharini samaki wenyewe wakimeza mifuko hii ya plastiki haiwezi kumeng’enywa na mwisho wake hufa,” alisisitiza.
Halikadhalika, Waziri Dkt. Kijaji alitoa wito kwa wafugaji nchini kuzingatia ufugaji ulio endelevu bila kuharibu mazingira ikiwemo kukata miti ovyo kwa ajili ya maja ni ya malisho.
Alibainisha kuwa malishio yanatoka kwenye mazingira na kwamba wafugaji wanahitaji malisho ya kudumu na endelevu ndio maana Serikali imeanza utaratibu wa kuwa na mbegu ambazo zimeshapata ithibati kwa ajili ya miti ya malisho.
Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inahamasisha kila mfugaji kuwa na eneo lake kwa ajili malisho na kuepuka kulisha mifugo kwa kuhamahama kwani kunachangia uharibifu wa mazingira
Kwa upande mwingine, Dkt. Kijaji alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya kazi nzuri ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu urejelezaji na utenganishaji wa taka na kuzitambua kuwa zinaweza kuwa ni mali kwa kutengenezea bidhaa na kulinda mazingira.
Kutokana na hatua hiyo alihimiza wananchi kuendelea kufanya usafi wa mazingira kuanzia nyumbani na hata maeneo ya kazi sanjari na kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu “Mazingira yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na Maisha.
Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani kitakuwa Juni 5, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.