Serikali yaongeza fedha kwa ajili ya kusomesha madaktari bingwa

0

Na WAF- DOM

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeongeza fedha za kusomesha Wataalamu bingwa na bobezi hadi kufikia Shilingi Bilioni 8 kutoka Shilingi Bilioni 3 za mwaka wa fedha 2021/22, utaosaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza Rufaa za nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya mmy Mwalimu Oktoba 28, 2022 wakati akitoa taarifa kuhusu mpango wa Serikali wa kuendeleza Watumishi wa Sekta ya Afya katika fani za ubingwa na ubingwa bobezi nchini uliopewa jina la “Samia Health Super Specialisation Programme.”

“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imeongeza fedha za kusomesha Wataalamu bingwa na bobezi hadi kufikia shilingi Bilioni 8 kutoka Shilingi Bilioni 3 za mwaka wa fedha 2021/22 utaosaidia kuboresha huduma za afya nchini. ” alisema Waziri Ummy.

Aliendelea kusema kuwa, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na bobezi nchini kuanzia mwaka huu wa fedha, Wizara imeanzisha mkakati mpya wa kutoa ufadhili kwa watumishi wa Sekta ya Afya kwa utaratibu wa set.

Utaratibu huu umeanzishwa ili kuhakikisha huduma za kibingwa zinazotolewa zinakuwa na wataalamu wote wanaohitajika ili huduma husika iweze kutolewa kwa ukamilifu, amesisitiza.

Aidha, Waziri Ummy alisema, Wataalamu watakaosomeshwa kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya figo kikamilifu katika set ni kama ifuatavyo; Daktari Bingwa wa Upasuaji figo, Daktari Bingwa wa matibabu ya figo, Daktari Bingwa wa utoaji dawa ya Usingizi kwa wagonjwa wa figo.

Daktari Bingwa wa Mionzi, Muuguzi Bingwa wa Mionzi, Mteknolojia Mionzi, Muuguzi Bingwa wa figo, Muuguzi Bingwa wa Usimamizi wa huduma za chumba cha upasuaji kwa wagonjwa wa figo na Mtaalamu wa Vifaa Tiba vinavyotumika kwa ajili ya matibabu ya figo, aliendelea.

Pia, Waziri Ummy alisema jumla ya watumishi 139 wamechaguliwa kupata ufadhili wa masomo ambapo kati ya hao 136 watasomeshwa nje ya nchi na 3 ndani ya nchi, ambapo Wizara itatoa ufadhili wa mafunzo ya set yaliyowasilishwa na Taasisi mbalimbali.

Sambamba na kufadhili watumishi 139 kwa utaratibu wa set pia watumishi 318 watafadhiliwa kwa utaratibu wa mtu mmoja mmoja na kufanya jumla ya watumishi watakaofadhiliwa kuwa 457 kwa mwaka wa fedha 2022/23, ambapo 146 (32%) ni wanawake. Kati ya watumishi 457 watakaofadhiliwa, 157 (34%) watasoma kwenye Taasisi za nje ya nchi.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali kuongeza fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 8 zitakazotumika kugharamia wataalamu waliochaguliwa kusoma mafunzo haya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here