Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
WATOTO 64 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum ya matibabu ya siku sita iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Watoto hao walikuwa na matatizo ya matundu pamoja na mishipa ya damu ya moyo ambapo 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 44 walifanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Upasuaji huo ulifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu jijini London nchini Uingereza kupitia mradi wake wa Little Heart.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia kambi hiyo ya siku sita serikali imeokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.6 fedha ambazo zingetumika kama watoto hao wengeenda kufanyiwa upasuaji huo nje ya nchi.
“Kupitia kambi hii madaktari wetu wameweza kujifunza mbinu mpya za kitabibu kwasababu shirika hili ilimekuwa likileta madaktari kutoka sehemu mbalimbali duniani hivyo kutuwezesha kupata ujuzi mpya waliona wenzetu,”.
“Tunamshukuru Rais wetu wa serikali ya awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye miundombinu na rasilimali watu katika Taasisi yetu hivyo kuifanya Taasisi hii kuwa na uwezo mkubwa katika kutoa huduma za kibobezi kwa watanzania wanaohitia huduma za matibabu ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi kujiunga na bima ya afya mara baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria ya bima ya afya kwa wote ili kukidhi gharama za matibabu pale watakapougua kwani magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo ni gharama kuyatibu.
Dkt. Kisenge alisema matibabu ya moyo yameigharamu fedha nyingi Serikali kusaidia jamii kwani wananchi wengi hawana uwezo wa kukidhi gharama za matibabu ya moyo kutokana na gharama zake kuwa kubwa lakini kama wananchi hao watajiunga na bima ya afya kutapunguza mzigo mkubwa ulioachiwa Serikali na kuiwezesha Taasisi hiyo kufanikisha matibabu ya watoto wengi zaidi.
“Upasuaji wa moyo kwa mtoto unagharimu shilingi milioni nane na kuendelea kama mtoto huyo atafanyiwa upasuaji hapa nchini lakini akipelekwa nje ya nchi itamgharimu kiasi cha shilingi milioni 25 kufanyiwa upasuaji, kama tutakata bima za afya itatusaidia kukidhi gharama za matibabu pale tunapopatwa na maradhi,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Meneja kutoka Shirika la Muntada Aid Kabir Miah alisema, kupitia mradi wa Little Heart unaotoa huduma mbalimbali zikiwemo huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo zaidi ya watoto 3000 kutoka maeneo mbalimbali duniani.
“Kupitia mradi wetu wa Little Heart tumefanya kambi za matibabu ya moyo zaidi ya 40 katika nchi 9 ambapo kwa hapa Tanzania hii ni mara yetu ya sita kuweka kambi ya matibabu ya moyo kwa watoto na jumla tumeshawafanyia upasuaji wa moyo watoto 416 tangu mwaka 2015 tulipoanza kushirikiana na Taasisi hii,”.
“Tunafurahi kushirikiana na wataalamu wa JKCI lakini pia tunawashukuru madaktari ambao wamekuwa wakijitolea kufanya kazi na shirika la Muntada Aid kutoka maeneo mbalimbali duniani lengo likiwa moja la kurejesha afya kwa watoto wetu ambao wanahitaji huduma ya matibabu ya moyo,” alisema Kabir.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Godwin Sharau alisema kila mwaka huduma za upasuaji zimekuwa zikiimarika kutokana na ujuzi ambao wamekuwa wakiupata kupitia kambi mbalimbali za matibabu zinazofanyika katika Taasisi hiyo.
“Ujuzi tunaopata kutoka kwa madaktari wenzetu unaongeza pia idadi ya watoto na watu wazima tunaowafanyia upasuaji wa moyo, mfano mwaka 2021 tulifanikiwa kufanya upasuji wa kufungua kifua kwa watoto 250 lakini kwa mwaka huu 2022 hadi sasa tupo mwezi wa kumi tumeshawafanyia upasuaji wa kufungua kifua watoto 230,”.
Kuhusu upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo Dkt. Godwin alisema kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) inapaswa kuwa na taasisi moja ya matibabu na upasuaji wa moyo ambayo itakuwa inatoa huduma kwa watu milioni 3 tu.
“Ukiangalia Tanzania sasa ina watu zaidi ya milioni 50 hii inamaanisha kwamba inahitaji kuwa na taasisi 20 za kutoa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu wanaozaliwa na matatizo ya moyo na kuhitaji huduma za matibabu hayo.
“Kutipita Taasisi yetu tumeweza kuzalisha wataalamu ambao ni mbegu tunayotaka kuisambaza Tanzania nzima ili huduma za matibabu na upasuaji wa moyo ziweze kufika katika mikoa yetu na kupunguza idadi ya watoto wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Godwin