Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu–Waso–Loliondo yenye urefu wa kilometa 211 kwa kiwango cha lami.
Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Akijibu swali la Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Yanick Ndoinyo, aliyetaka kujua ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika, Eng. Kasekenya amesema kuwa sehemu ya Waso–Sale yenye urefu wa kilometa 49 tayari imekamilika kwa kiwango cha lami.
Aidha, Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Waso–Loliondo chenye urefu wa kilometa 10, huku taratibu za malipo ya awali kwa wakandarasi zikiendelea.
Ameongeza kuwa taratibu za manunuzi kwa ajili ya kuwapata wakandarasi wa ujenzi wa sehemu ya Mto wa Mbu–Selela (km 23) na Selela–Engaruka (km 27) zinaendelea, huku Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha sehemu zilizobaki za mradi huo.
“Serikali pia ina mpango wa kujenga kiwanda cha magari katika ukanda wa barabara ya Mto wa Mbu–Engaruka hadi Loliondo, eneo ambalo ni muhimu kiuchumi na kimkakati kwa kuimarisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi,” amesema Eng. Kasekenya.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amemhakikishia Mbunge wa Tunduru Kusini, Mhandisi Chilombe, kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tunduru Mjini hadi Chateka kwa kiwango cha lami.
Pia, Serikali inaendelea kubaini na kuboresha maeneo korofi ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika katika kipindi chote cha mwaka