Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imedhamiria kuboresha na kujenga barabara nyingi za wilaya ili kurahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Hadi sasa, mtandao wa barabara za Wilaya umeongezeka kutoka Kilomita 108,946.19 hadi Kilomita 144,429.77.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seiff wakati akizungumza katika Kikao kazi na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere JNICC jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seiff alisema, hadi kufikia Juni, 2024 Barabara za lami za wilaya zilikuwa Kilomita 3,337.66 sawa na asilimia 2.31, kati ya hizo, Kilomita 2,743.81 zipo katika hali nzuri, Kilomita 445.18 zipo katika hali ya wastani na Kilomita 148.68 zipo katika hali mbaya.
“Kwa upande wa changarawe hadi kufikia Juni mwaka huu, barabara za wilaya zimefikia Kilomita 42,059.17 na lami Kilomita 3,0337.66” alisema na kuongeza, “Wilaya ya Rufiji zimejengwa Kilomita 32 kwa kutumia teknolojia ya kokoto (Ecozyme) na Wilaya ya Itilima Kilomita 5.2,”
“Tunatumia malighafi kama mawe ambayo hupunguza asilimia zaidi ya 50 ya gharama na tayari tumejenga madaraja 275 na Kilomita 225 za barabara kwa kutumia mawe,” alisema Seif.
Alisema, kwa kutumia teknolojia hiyo jiji la Dodoma tayari Kilomita moja imejengwa na Wilaya ya Chamwino Kilomita 6.95 na zote zimekamilika. “Tathimini iliyofanyika mwaka 2022/2023 ilibaini Shilingi Trilioni 1.35 zinahitajika kuanzia 2023/2024; ili asilimia 85 ya mtandao wa barabara za wilaya zipitike misimu yote, sasa TARURA inapata wastani wa Shilingi. Bilioni 850 kwa mwaka,”
Aidha, kwenye mkutano huo na wahariri, Mhandisi Seiff alielezea mradi wa uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDPi II), ambao unalenga kuboresha maeneo mengi ya jiji hilo.
Alisema, mradi huo utakuwa ndani ya Halmashauri tano za jiji la Dar es Salaam na utatekelezwa kwa miaka sita na utahusisha ujenzi wa barabara Kilomita 250 mifereji Kilomita 90, vituo vya mabasi tisa, masoko 18 na madampo matatu.
Mbali na mradi huo, ujenzi mwingine ni daraja na uendelezaji wa Mto Msimbazi, ambapo alisema eneo la chini la mto huo linatarajiwa kuongezwa kina na kupanuliwa ili kuruhusu maji kwenda Baraharini kwa kasi inayotakiwa.
“Mradi huu umeanza rasmi tarehe 16 Februari 2023 na unatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola za Marekani Milioni 200), Serikali ya Hispania (Euro Milioni 30) na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi (Euro 30).
“Hadi sasa asilimia 98 ya watu ambao wanaathirika na mafuriko wamelipwa fidia na wameondoka, lakini zipo kaya takribani 314 ambazo zimetambuliwa kuwa zitaathirika na ujenzi na mchakato wa kuandaa daftari la fidia unaanza mwezi Septemba mwaka huu,” alisema Mhandisi Seiff.