WAZIRI wa Nchi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amelieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa kuratibu masuala ya Muungano na Yasiyo ya Muungano (UNUMMiS).
Akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026, Waziri.
Masauni alisema, mfumo huo umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na utendaji kazi ambapo kwa sasa upo katika hatua za majaribio ili kuona kama unakidhi matakwa ya watumiaji na pindi utakapokamilika utasaidia wananchi kufahamu kwa kina masuala muhimu yanayohusu Muungano.
Aidha, Masauni alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuratibu masuala ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha Wizara/Idara na Taasisi zinafanya vikao vya ushirikiano.
Aliongeza kuwa, hadi kufikia mwezi Machi 2025 jumla ya vikao vinane vya ushirikiano vilifanyika vilivyolenga katika kubadilishana uzoefu, Sera, Sheria na utaalamu katika utekelezaji wa mambo yasiyo ya Muungano.
Mhandisi Masauni alisema, katika kuimarisha sekta ya hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni imesajili jumla ya Miradi 73 ya Biashara ya Kaboni ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Aliongeza kuwa, Biashara ya kaboni imeanza kuleta manufaa kiasi katika baadhi ya maeneo nchini ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 45 zimelipwa na kunufaisha wananchi katika Halmashauri 10 nchini kama gawio la mauzo ya viwango vya kaboni.
“Ofisi iliratibu vikao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao cha kuwajengea uwezo Makatibu Wakuu 21 kuhusu biashara ya kaboni, Wawakilishi wa Makampuni 27 yanayojihusisha na biashara ya Kaboni, Vikao vya kimkakati vya kuimarisha usimamizi wa biashara ya Kaboni baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara za kisekta,” alisema Waziri Masauni.