Serikali yaagiza Magereza kupewa ruzuku ya nishati safi ya kupikia

0

đź“Ś Dkt. Biteko atoa mabati 300 ujenzi wa darasa Chuo cha Mafunzo

đź“Ś Magereza yapongezwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia

đź“Ś Dkt. Samia apongezwa kwa kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameilekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoa ruzuku kwa Jeshi la Magereza ili kutekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuhakikisha Magereza yote yanaondokana na Nishati isiyo safi.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo leo Machi 28, 2025 jijini Dar es salaam katika hafla ya kufunga Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Namba 27 – 2024/2025 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA).

“Magereza yote 129 yamehama katika matumizi ya kuni na sasa yanatumia nishati safi ya kupikia. Naielekeza REA ile ruzuku tunayopanga kuitoa kwa wazalishaji mbalimbali kwa ajili ya vifaa vya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Magereza wapewe kipaumbele,” alisema Dkt. Biteko.

Amewapongeza wahitimu hao wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Namba 27 – 2024/2025 na kusema kuwa ni mategemeo ya Serikali na jamii kuona wanakuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi na kuimarisha mshikamano katika Jeshi la Magereza.

“Mkuu wa Chuo ametuthibitishia kuwa mmefanya vizuri katika mafunzo yenu. Na mmekidhi vigezo vya kupandishwa cheo na Mamlaka husika kuwa Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Magereza. Hongereni sana kwa hatua hii kubwa, pamoja na pongezi hizi naomba niwakumbishe kupandishwa cheo ni kuongezewa majukumu,” alieleza Dkt. Biteko.

Pamoja na hayo amewataka wahitimu hao kuwasikiliza na kuwatendea haki kwa askari walio chini yao sambamba na kuwawajibisha wavivu na kuwatia moyo wachapakazi.

Vilevile, Dkt. Biteko ametoa rai kwa wahitimu hao kujiendeleza kielimu na kufanya kazi kwa bidii ili Jeshi la Magereza kuwa la mfano na kutoa huduma bora kwa Watanzania ili kufikia matarajio ya Serikali.

“Kamishna wa Jeshi la Magereza endelea kuwaunganisha na kuweka pamoja askari, Serikali inatambua kazi unayofanya na mchango wako kwa Taifa, Serikali inatambua mchango wa Chuo hiki kwa askari wote, alisema Dkt. Biteko.

Akizungumzia Haki Jinai, Dkt. Biteko alisema “Niuombe uongozi wa Jeshi, kuendelea na jitihada za kuboresha utendaji kazi ndani ya Jeshi katika nyanja mbalimbali na utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuboresha Haki Jinai ili kulifanya Jeshi liendane na wakati kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.“

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amechangia mabati 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa darasa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania.
 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Vicent Mbogo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha vyombo vya usalama ikiwemo Magereza. Pia amempongeza Mkuu wa Magereza kwa kuwa na ubunifu wa kuwapeleka wafungwa katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ambapo huwasaidia kupata ujuzi mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu kwa kusaidia mkoa huo kuendelea kuwa salama.

“Tunamshukuru Kamishna Jenerali kwa mchango mkubwa anaoutoa katika mkoa wetu wakati wa shughuli mbalimbali, hata Maafisa hawa waliohitimu leo wamekuwa na mchango katika kusaidia usalama wa Mkoa huu,” alisema Mpogolo.

Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu alisema, hali ya magereza nchini ni shwari na kuwa Jeshi hilo limeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.

Alisema, Magereza 66 yana huduma za Mahakama Mtandao na kuwa tayari wamepokea Shilingi Milioni 668.8 kwa ajili ya kujenga Magereza Mtandao katika Magereza yote nchini ili kusaidia upatikanaji haki kwa wakati.

“Nawashukuru na kuwapongeza wahitimu wote, utendaji wenu wa kazi uakisi yale yote mliyojifunza katika nyanja mbalimbali na Jeshi halitaacha kuchukua kwa yeyote atakayekiuka,” alisema Kamishna Jenerali Katungu.

Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), SACP Wilnton Kahumuza amesema Mafunzo hayo ya Uongozi Ngazi ya Juu Na. 27 yalianza Novemba 30, 2024 yakiwa na idadi ya wanafunzi 203.

Aliendelea kusema, Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia wanafunzi ujuzi mbalimbali ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Jeshi kwa kadri itakavyohitajika.

“Wahitimu wanaohitimu leo wamefanya mafunzo ya darasani na wanastahili kupandishwa cheo kwa masomo waliyosomea,” alisema SACP Kahumuza.

Pia, amewashukuru wahitimu hao kwa kuonesha kujituma na kuwa na moyo wa kuchanga fedha shilingi 7,703,200 kwa ajili ya kujenga mnara wa tenki la maji na kununua tenki lenye ujazo wa lita 5,000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here