SERIKALI inajenga bandari nyingine nje ya Manispaa ya Mtwara Mikindani itakayotumika kusafirisha bidhaa chafuzi kwa mazingira kama vile saruji na makaa ya mawe, ili magari yote yanayobeba makaa ya mawe kupita nje ya manispaa kuelekea bandarini.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis alisema hayo bungeni jijini Dodoma leo Juni 25, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Malapo, aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kudhibiti vumbi la makaa ya mawe yanayosafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais zinashirikiana kutekeleza mradi huo katika eneo la Kisiwa Mgao.
Alisema, katika kutekeleza mradi huo itatumika mitambo miwili yenye uwezo wa kupakia tani 600 kwa saa ambayo ina mikanda maalum (conveyor belt) kwa ajili ya kupakia mzigo kwenye meli.
Khamis alitaja hatua nyingine ni kuweka nyavu za kuzuia vumbi, kuhakikisha magari yote yanayosafirisha makaa ya mawe yanafunikwa ili kuzuia vumbi lisisambae kwenye mazingira na kunyunyuzia maji mara kwa mara katika eneo la hifadhi.