NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Zainab Katimba amesema Serikali inafahamu itaendelea kuajiri walimu wa masomo ya sayansi nchini kutokana na mahitaji ya maeneo husika.
Katimba ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Buchosa Eric James Shigongo. aliyeuliza Je, Serikali inafahamu tatizo la uhaba wa Walimu hasa wa Masomo ya Sayansi nchini?
“Serikali imekuwa ikiajiri walimu wa kada mbalimbali ikiwemo walimu wa masomo ya sayansi kadiri ya upatikanaji wa fedha. Mwaka 2024/25 Serikali imeajiri walimu 15,925 wakiwemo walimu 5,115 wa masomo ya sayansi ambao wamepangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu zaidi.” alisema.
Alisema, sensa ya Elimu Msingi Mwaka 2024 inaonesha kuwa mahitaji ya walimu wa masomo ya sayansi ni 31,123 waliopo ni 21,309 na upungufu ni walimu 9,814, Serikali itaendelea kuajiri walimu wa masomo ya sayansi kadiri ya upatikanaji wa fedha.