Rushwa, ukiukwaji wa sheria ya ununuzi wa umma kukoma

0
Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi.

Na Yussuf Abbas, Dodoma

KATIKA hatua za kuboresha Sekta ya Ununuzi wa Umma nchini, Serikali imetunga sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma inayotarajiwa kuanza kutumika hivi karibuni.

Maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 yaliyofanyika hivi karibuni yamelenga kuleta chachu kubwa katika sekta kwa kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na thamani ya fedha inapatikana katika michakato ya ununuzi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Eliakim Maswi amesema yapo mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika Sheria mpya ukilinganisha na Sheria iliyopo sasa.

“Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa sikivu, maisha ya Mtanzania katika ununuzi wa Umma sasa yanabadilika, kilio cha muda mrefu cha rushwa na ukiukwaji wa sheria katika ununuzi wa umma sasa kimepatiwa ufumbuzi,” alisema

Moja ya mafanikio makubwa katika sheria hii mpya ni pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa wazabuni wazawa kwa kuwawekea upendeleo wa kushinda zabuni katika zabuni zenye ushindani wa Kimataifa.

Upendeleo huo unahusisha zabuni za baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa, zilizochimbwa au kuzalishwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi za ujenzi za wakandarasi au huduma zilizotolewa na washauri elekezi watanzania.

“Miongoni mwa vigezo vya jumla vilivyowekwa kwa upande wa wakandarasi au washauri elekezi ili kupata upendeleo wa zabuni za kitaifa kwa kampuni binafsi au ushirika wa kampuni za ndani ni pamoja na kigezo cha kampuni hizo kuwa zimeanzishwa au kusajiliwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu kubwa ya mtaji wa hisa zilizolipwa za kampuni binafsi iwe inamilikiwa na raia wa Tanzania,” alisema

Aliongeza kuwa, kigezo kingine ni pamoja na kampuni hizo zisiwe na utaratibu unaoelekeza sehemu kubwa ya faida halisi kutolewa au kulipwa kwa watu ambao si raia wa Tanzania au kwa kampuni ambazo zisingekuwa na sifa chini ya kifungu husika.

Aidha, Maswi aliongeza kuwa, Sheria hiyo pia imeweka upendeleo wa kipekee kwa watu au kampuni za ndani kwa kuzitaka taasisi nunuzi kutenga kiasi cha bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya watu au kampuni za ndani pekee kwa kila ununuzi wa kazi za ujenzi, bidhaa au huduma wenye thamani isiyozidi ukomo utakaoainishwa katika kanuni.

“Utekelezaji wa suala hili utakuja endapo taasisi nunuzi imepokea ofa moja tu inayokidhi vigezo kutoka kwa mtu au kampuni ya ndani katika ununuzi uliotengwa, taasisi nunuzi inaweza kutoa tuzo kwa mtu au kampuni hiyo,:

“Pia, endapo taasisi nunuzi haijapokea ofa zinazokidhi vigezo kutoka kwa watu au kampuni za ndani, inapojitokeza hali hii ununuzi uliotengwa utaondolewa na ikiwa vigezo bado viko halali, ofa mpya zitatangazwa kwa mara nyingine kwa misingi isiyo ya upendeleo.” alibainisha Maswi.

Maeneo mengine ya upendeleo yaliyozingatiwa katika Sheria hii ni pamoja na eneo la matumizi ya wataalamu wa ndani katika mikataba ya kazi za ujenzi na huduma zisizo za kitaalamu, Upendeleo kwa bidhaa za ndani, Uingiaji wa ushirika au mikataba midogo na kampuni za ndani pamoja na Upendeleo wa utoaji zabuni kwa makundi maalum ya kijamii.

Maboresho haya ya Sheria ya ununuzi wa umma, Sura 410 yanaenda sambamba na ujenzi wa mfumo mpya wa ununuzi wa umma kielektroniki (NeST) unaoendelea kuongeza ufanisi katika sekta ya ununuzi nchini tangu ulipoanza kutumika miezi michache iliyopita mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here