Rais Samia azindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

0

Na Mwandishi wa OMH

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kufikia lengo kuu la kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi, la haki na linalojitegemea.

Rais Dkt. Samia aliyasema hayo Alhamis, Julai 17, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa Dira uliofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), tukio ambalo pamoja na viongozi wengine lilihudhuriwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Aidha, Rais Dkt. Samia alisema Dira 2050 ni matokeo ya mchakato jumuishi uliohusisha maoni ya wananchi na wadau wote na inalenga kufanikisha maendeleo jumuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Rais Dkt. Samia alisema Dira hiyo iliyozingatia matarajio ya Watanzania imejengwa juu ya msingi wa mafanikio na mafunzo ya historia ya maendeleo ya Tanzania tangu Uhuru, ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa Dira ya 2025.

“Maudhui ya Dira 2050 yametokana na maoni na matakwa ya Watanzania wenyewe. Tumefikiri wenyewe, tumeandika wenyewe, tumepanga wenyewe na tutatekeleza wenyewe,” alisema Rais.

Rais Dkt. Samia alisema kuwa uandaaji wa Dira hii umezingatia muktadha wa sasa wa dunia unaogusa masuala muhimu kama vile mabadiliko ya mfumo wa uchumi wa dunia, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko kubwa la vijana nchini na mapinduzi ya kiteknolojia.

Aliongeza kuwa, kwa ukubwa wa rasilimali, ari na uwezo wa wananchi, Tanzania ina kila sababu ya kuweka na kufikia malengo makubwa ya maendeleo iliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na lengo kuu la kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu yenye uchumi wa $1 trilioni ifikapo mwaka 2050.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here