RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usajili kidijitali wa matukio ya kijamii kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Agosti 10, 2025 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usajili Barani Afrika yaliyofanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi unaofanywa na Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) katika usajili wa vizazi, vifo, talaka, ndoa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Rais Dkt. Mwinyi alisema, hakuna maendeleo ya kweli bila usajili wa utambulisho wa wananchi katika mifumo imara inayotambulika kisheria na inayotumia teknolojia ya kisasa ya kidijitali.
Aidha, Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa ZCSRA kuanzisha kampeni maalum kwa kushirikiana na masheha kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa wanapata vyeti vya kuzaliwa kisheria ifikapo mwaka 2030.
Amefafanua kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Lengo la 16 miongoni mwa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, linalosisitiza kila mtu kupata utambulisho wa kisheria katika nchi yake.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi alisema usajili wa matukio ya kijamii una umuhimu mkubwa katika kufanikisha mipango ya Serikali, kuimarisha ustawi wa jamii, kupata takwimu sahihi kwa taasisi zinazotoa huduma, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ajira, huduma za afya, elimu na upangaji wa bajeti za maendeleo.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni jambo la kujivunia kuona mifumo ya usajili nchini inasomana na mifumo mingine ya utoaji huduma kwa jamii, hatua inayoongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na kuondoa urasimu.