Rais Mwinyi: Shirika la viwango duniani endeleeni kuisaidia ZBS

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amelishukuru Shirika la Viwango Duniani (ISO) kwa kuendelea kulijengea uwezo Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS), hatua inayolisaidia kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa shirika hilo, ukiongozwa na Rais wake, Dkt. Sung Hwan Cho, uliofika Ikulu kwa mazungumzo Juni 24, 2025.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa shirika hilo kufanya kazi kwa ukaribu na ZBS pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuhakikisha taasisi hizo zinatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa katika kusimamia ubora wa viwango.

Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amelishauri ISO, kuendeleza misaada ya kitaalamu kwa taasisi hizo pamoja na kuwajengea uwezo watendaji wao, ili kuwaongezea taaluma na ujuzi unaohitajika katika sekta ya viwango.

Rais Dkt. Mwinyi amelipongeza shirika hilo kwa uamuzi wake wa kushiriki kikamilifu katika Mkutano Mkuu wa Viwango Afrika, unaotarajiwa kufanyika Zanzibar kesho tarehe 25 Juni 2025.

Naye Rais wa ISO, Dkt. Sung Hwan Cho, amesifu ushirikiano uliopo baina ya shirika hilo na ZBS na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake, Rais wa Shirika la Viwango Afrika (ASO) ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Viwango la Ghana, Prof. Alex Doddoo, alisema umefika wakati kwa Afrika kuwa na viwango vyake vyenyewe ili kukabiliana na vikwazo vya kibiashara duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here