Rais Mwinyi ni chuo cha uongozi

0

Na Derek Murusuri

MWAKA 1993 tulikuwa tunahitimisha ziara ya Rais Ali Hassan Mwinyi, Mkoani Shinyanga. Mara, tukaambiwa Rais anataka kupiga picha na wapiga picha wake.

Lol, sisi? Mbio tukaenda. Akatusalimia kwa kutushika mkono, akitushukuru kama baba kwa mwanaye. Alifurahia jinsi habari zake na hasa picha, zilivyokuwa zikipigwa na kuchapishwa katika magazeti mbalimbali hapa nchini. Alikuwa mtu wa kushukuru.

Nami nilikuwa mmoja wa wapigapicha kutoka Idara ya Habari, MAELEZO. Bosi wangu, Raphael Hokororo alinipanga kwenye ziara hiyo. Rais Mwinyi akatuita, “Njooni tupige picha ya ukumbusho.” Hima tukajongea. Akiwa na Mama Sitti Mwinyi, waliketi, sisi wapiga picha tukasimama nyuma yao.

Mpiga picha mmoja akatupiga picha sisi wapiga picha, pamoja na Rais na mkewe. Baada ya zoezi hilo, akatuaga. Sio viongozi wote wanaojua kushukuru. Yaani, Rais anakushukuru kwa kutekeleza wajibu wako. Tena Kiongozi Mkuu wa Taifa. Halafu wewe ni mpiga picha tu.

Mwaka huo huo, nilifanya naye kazi Ikulu kwa wiki mbili na ushee hivi, chini ya Balozi Patrick Chokala. Kipindi hicho, mpiga picha wake, Mzee Henry Isike, alikuwa likizo. Wakubwa wangu pia, walikuwa safari. Nilipomuomba asogee hivi ili picha itoke vizuri, alikubali kwa unyenyekevu mkubwa sana.

Nikiwa Tume ya Mipango, iliyokuwa chini ya ofisi ya Rais; Rais Mwinyi ndiye aliyekuwa Mwenyekiti. Niliwahi kuhudhuria kikao kimoja cha tume hiyo katika chumba cha Baraza la Mawaziri, Ikulu, nikashuhudia hekima yake kubwa ya kuendesha vikao. Alimsikiliza kila mwenye hoja, tena kwa umakini mkubwa.

Alikuwa kiongozi mnyenyekevu sana, mvumilivu, mwana mageuzi, aliyeujenga upya uchumi wa Tanzania, baada ya kuharibiwa sana na vita ya Kagera na hata vita ya harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Naweza kusema kuwa, Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa Deng Xiaoping wa Tanzania, kwa kipindi kile, kuanzia mwaka 1985. Deng ndiye Baba wa Uchumi wa China.

Mafanikio ya China ya leo, kutoka Taifa la ulimwengu wa tatu hadi kuwa Taifa lenye uchumi wa pili mkubwa zaidi duniani, yanatoka kwa Deng Xiaoping, aliyeingia madarakani mwaka 1978.

China leo hii, inaweza kuipiku Marekani kama Taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani, wakati wowote. Rais Mwinyi, alifanya kazi sawasawa na Deng kwa China. Watanzania hawana budi kumpatia nafasi yake stahiki. Ninaamini TUZO ziko njiani, hata kama atakuwa kaburini.

Mwaka 2009, wakati akihutubia Baraza la Maulid, kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, alipigwa kofi na kijana mmoja, na alipatwa na tukio hilo kwa vile alikuwa anajichanganya na raia; licha ya shambulizi hilo, Mzee Mwinyi alimsaheme kijana yule.

Hata wakati akiwa Rais na Amir Jeshi Mkuu. Majeshi ya ulinzi na usalama vilikuwa chini yake, aliwahi kuwasamehe mahasimu wake. Kwa nafasi aliyonayo, hata kama Mahakama ni mhimili tofauti, lakini angeweza kushawishi ili mahasimu wake waadhibiwe, lakini hakuitumia nafasi yake wala maguvu yake kuwashikisha adabu mahasimu hao.

Yeye alikaa kimya. Akasamehe. Tena akafanya nao kazi ili aujenge upya uchumi wa Taifa la Tanzania. Akachapa kazi. Akawaamini watu. Hakuchukua maguvu yote peke yake. Nchi ikasimama.

Rais Mwinyi wakati anaingia madarakani alikuta foleni za kununua sembe, dawa za meno na sabuni zilikuwa adimu na zilipatikana kwa magendo. Alikuta watu wanafulia nguo zao sabuni za MAGWANJI, wenye bahati ya kuwa na mipapai, wakatumia majani yake kufulia nguo zao, lakini baada ya muda mfupi bidhaa zote hizo zilijaa madukani.

Mzee Ali Hassan Mwinyi ni chuo. Yapo mengi sana ya kujifunza kutoka kwake. Hakika, alikuwa kiongozi makini na alijitoa sana kwenye mambo ya kijamii. ‘Power Distance’ kwake ilikuwa kidogo. Yaani, alikuwa karibu na raia aliowaongoza.

Mbali na kufanya mazoezi ya kutembea kila siku, huenda ndiyo siri ya kuishi miaka 98 na miezi 9, takriban miaka 99, alijaaliwa na Mola wake kwa kuonesha maisha ya msamaha, alifundisha Kiswahili kwa kujitolea nchini Uingereza.

Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa zamani wa Afrika Mashariki, ambaye ni mmoja wa vijana wa Mzee Mwinyi, alipata kunieleza tukiwa Cardiff University, kuwa wakati Mzee Mwinyi akiwa Uingereza, alijitolea kufundisha Kiswahili kwa bidii sana.

Ndio maana, BAKITA na vyombo vya habari vilimtumia vizuri hapa nyumbani. Alijua, tukiwa na lugha yetu, ikakua na kutumika hata kwenye Sayansi, Taifa litapata maendeleo makubwa.

Hili ni somo kubwa sana la unyenyekevu katika uongozi kwa Watanzania na waafrika wote. Nadhani sio kwa viongozi wa kisiasa pekee, nahisi ni katika maisha ya kila mmoja wetu. Nyumbani, ofisini, katika jamii na Taifa.

Hata Nabii Issa Bin Maryam, Bwana Yesu Kristo, alijishusha na kunyenyekea sana. Kuna nyakati alinyamaza pasipo kusema neno lolote. Hakutumia uwezo wake wa kiungu kuwasaga adui zake.

Nimeamini, Mwenyezi Mungu huwapenda watu wanyenyekevu, wenye huruma na wacha Mungu. Basi, ngoja Kiongozi wetu, Mzee wetu, Baba yetu, Rafiki yetu, apumzike kwa amani. Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, hakika aliutumia vizuri muda wake hapa duniani.

Kumbe ‘humility’ ni msingi mkuu wa kiongozi bora na namna njema ya kuishi hapa duniani. Hata alipolazimika kujiuzulu, ilifika mahali yeye na familia yake wakapatiwa hifadhi na rafiki wa karibu. Hakuwa mbadhirifu. Alikuwa mwadilifu. Lakini, hakujisikia vibaya. Muda ulipofika, Mwenyezi Mungu akamkumbuka. Alikuwa mvumilivu sana.

Huyu Kiongozi wetu aliyeondoka hakika alikuwa binadamu wa pekee sana. Nilifurahi kumuona, yeye na mke wake, Mama Sitti, wakitumia usafiri wa Daladala, Mwendo kasi. Nilifurahi sana. Hii ni ishara ya unyenyekevu. Hakuongelea unyenyekevu, maisha yake yalitangaza unyenyekevu.

Tena siku hiyo haikutangazwa kwenye vyombo vya habari kuwa Mzee Mwinyi atatumia usafiri wa Mwendo kasi, alifurahi kusafiri na Wananchi wa kawaida aliowaongoza. Alipenda maendeleo.

Alijaaliwa kipaji cha hekima kubwa. Kwa kweli ameacha funzo kubwa kwenye kada ya uongozi katika Bara la Afrika. Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi, amjaaliye Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, pumziko la amani, hadi tutakapoonana ya pili.

INNA LILLAHI WA INNA ILAYHI RAJIUN!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here