Rais Mwinyi na vita ya viongozi wadhalilishaji

0

Na Reubeni Lumbagala

UDHALILISHAJI wa wanawake na watoto ni ukatili ulioshamiri katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Udhalilishaji huo ni kinyume kabisa na tamaduni, imani, miongozo, sheria na kanuni za nchi yetu.

Kutokana na kushamiri kwa vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, Serikali na taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs) zimeweka mikakati mbalimbali ya kupambana na ukatili huu ikiwemo hatua ya kuwafikisha wahusika wa ukatili huo katika vyombo vya sheria kwa hatua za kisheria.

Visiwa vya Unguja na Pemba ni miongoni mwa maeneo ambayo vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto vimeshamiri, hali inayohatarisha ustawi wa wanawake na watoto na maendeleo kwa ujumla.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametangaza vita rasmi kwa watendaji na viongozi watakaobainika kushiriki vitendo vya udhalilishaji kwani wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuleta matokeo chanya ya mapambano haya kwa ustawi wa watu na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Rais Mwinyi alisema hayo katika hafla ya kuipongeza Taasisi ya The Foundation for Civil Society (FCS) kutokana na mchango wake wa kupinga ukatili wa kijinsia katika kongamano la harakati za kutokomeza vitendo vya udhalilishaji lililoandaliwa na Taasisi ya ZEFELA. Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Rais Mwinyi alisema, hatosita kumchukulia hatua mtendaji yeyote aliyemteua ambaye atabainika kujihusisha na vitendo vya udhalilishaji. Vilevile, Rais Mwinyi ameonyesha kusikitishwa kwake na baadhi ya wateule wake kuwa washirika wa vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua stahiki.

Waziri Mwinyi alisema “Ukiyasikia haya yanasemwa hapa mimi binafsi napata huzuni kubwa kwa sababu inaonekana taasisi zinazotakiwa kufanya kazi zao hazifanyi na zina watu wanajulikana, lakini wapo wanaendelea kutizamwa bila ya kuchukuliwa hatua.”

Watendaji na viongozi wamepewa dhamana kwa ajili ya kusimamia taratibu, sheria na kanuni, ili dunia iwe sehemu nzuri ya kuishi na kuwe na ustawi nzuri wa maisha ya watu na kufikia malengo ya Taifa.

Baadhi ya watendaji na viongozi wanaposhindwa kusimamia wajibu wao wa msingi wa kufanya hivyo, ni dhahiri wanakuwa wameshindwa katika nafasi walizoaminiwa na mamlaka za uteuzi na kuchaguliwa na wananchi, na hivyo, hawana budi kupisha wengine wenye uwezo wa kusimamia majukumu yao ipasavyo.

Taifa haliwezi kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa kama kundi hili muhimu la wanawake na watoto wanaendelea kufanyiwa ukatili na udhalilishaji. Ni dhahiri ukatili na udhalilishaji unarudisha nyuma maendeleo ya kundi hili muhimu (wanawake na watoto) na hata maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Watendaji na viongozi wana wajibu wa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mapambano haya ili kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili na udhalilishaji kama kupiga wanawake, ubakaji na ukatili wa watoto ambao ni kikwazo katika upatikanaji wa maendeleo ya nchi.

Aidha, Rais Mwinyi ameonyesha kusikitishwa kwake na vitendo vya wanaume kuwapiga wake zao. Rais Mwinyi amekemea tabia hiyo na kuwaasa wanaume kuacha tabia hiyo kwani hata imani za dini zina utaratibu wake katika suala la mwanaume kumpiga mke wake.

“Wapo wanaume ambao wanawapiga wake zao halafu wakija mnaambiwa kawaida tu lakini dini zinatuambia unapotaka kumpiga mke basi upo utaratibu unaotuelekeza” alisema Rais Mwinyi.

Taasisi ya The Foundation for Civil Society (FCS) imeatoa mchango mkubwa Zanzibar katika mapambano ya ukatili na udhalilishaji ili kuleta ustawi na maendeleo katika visiwa vya Pemba na Unguja.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga amesema “Miongoni mwa kazi kubwa iliyofanywa na FCS Zanzibar kwa miaka mitano iliyopita ni pamoja na kutoa ruzuku yenye thamani ya Sh. 4,094,639,230 kwa mashirika 73 yanayofanya kazi katika sekta za maboresho ya sera, haki, za ardhi kwa wanawake, kupinga ukatili wa watoto,”

Ushiriki na ushirikiswaji wa jamii katika maendeleo, ajira kwa ijana, ujenzi wa amana na utatuzi wa migogoro, kuchangia katika mchakato wa uaandaji wa rasimu ya sheria ya NGO’s kwa ufadhili zoezi la ukusanywaji wa maoni ya wadau na Jumuiya kutoka Pemba na Unguja.”

Pamoja na kwamba watendaji na viongozi wana jukumu la kusimamia kikamilifu mapambano ya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji, bado mchango wa wananchi ni muhimu sana katika kufikia matokeo chanya ya mapambano haya.

Kimsingi, ukatili na udhalilishaji unafanyika ndani ya familia na jamii, hivyo jamii inapaswa kuwafichua wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwani kwa kufanya hivyo, jamii itapata funzo na kuachana na tabia hiyo, hatimaye kuyafikia maendeleo ya kweli.

*Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali ya wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma. Maoni: 0620 800 462.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here